Waogeleaji wanne kwenda Kenya leo

DAR ES SALAAM;  WAOGELEAJI wanne wa timu ya taifa wanatarajiwa kuondoka leo kwenda Nairobi nchini Kenya kushiriki mashindano ya taifa yatakayoanza Juni 22-23, mwaka huu.

Timu hiyo inakwenda kwenye mashindano hayo kama mwalikwa. Akizungumza na waogeleaji hao Dar es Salaam jana wakati akiwakabidhi bendera ya Taifa, Ofisa Michezo wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Abel Odena aliwataka kwenda kupambana kuhakikisha wanarudi na medali nyumbani.

“Nendeni mkapambane na kuhakikisha mnaipeperusha vema bendera ya Taifa kwa kupata medali nyingi za dhahabu kwani kila kitu kinawezekana,” alisema Odena.

Isome pia:https://habarileo.co.tz/tanzania-yachomoza-kimataifa-kuogolea/

Kwa upande wake Kocha Mkuu wa timu hiyo, Alexander Mwaipasi alisema watakwenda kushindana
kwa kutumia bwawa la mita 50.

“Tumejipanga vizuri kuhakikisha tunakwenda kufanya vizuri katika mashindano hayo ambayo naamini yatakuwa na ushindani kwa kuwa wachezaji wetu wamezoea kuogelea kwenye bwawa la mita ishirini na tano,” alisema Mwaipasi.

Aliwataka Watanzania kuwaombea ili waweze kutimiza malengo yao katika michuano hiyo itakayoshirikisha klabu mbalimbali.

Aliongeza kuwa waogeleaji watatu watacheza mbio nane na mmoja atacheza mbio saba. Naye Meneja wa timu hiyo, Francisca Binamongo alisema wamewaandaa vema waogeleaji kwa kuwapa mazoezi ya nguvu ili warudi na ushindi.

Nahodha wake Romeo Mihaly alisema licha ya kuwa wamezoea kuogelea kwenye bwawa la mita 25, hakuna kitakachowazuia wasifanye vizuri na badala yake watatumia maelekezo waliyopewa na viongozi kufanya vizuri.

Habari Zifananazo

Back to top button