Hans Rafael atoa tathmini ubora wa Simba SC

DAR ES SALAAM: MCHAMBUZI maarufu wa Michezo nchini, Ansibert Rafael ‘Hans Rafael’ ametoa tathmini yake kuhusu Simba SC kushindwa kurudisha ubora wao ndani ya ligi na michuano ya kimataifa pia.

Akitoa tathmini yake kupitia mtandao huu wa HabariLeo mapema leo Aprili 15, Hans Rafael amesema changamoto kubwa ya Simba SC ni kukosa muendelezo wa kikosi tangu ilipotwaa ubingwa wa msimu wa 2020/2021.

Amesema tangu msimu huo, timu hiyo imeshindwa kujenga kikosi cha muda mrefu, hali iliyowalazimu kusajili wachezaji wengi kila msimu, kati ya 7 hadi 10 katika madirisha yote mawili ya usajili.

“Tatizo hili limeathiri uthabiti wa timu, hasa kutokana na kusajili wachezaji wasiokuwa na ubora unaohitajika, ambapo baadhi yao wamekuwa wakicheza kwa muda mfupi wa miezi sita kisha kuondoka,” amesema Hans Rafael.

Aidha, aliwataja Pa Omar Jobe na Babacar Sarr kuwa ni wachezaji ambao walisajiliwa klabuni hapo, ila walishindwa kudumu na timu hiyo, huku karibia kikosi kizima kikivunjwa na kuanza upya msimu huu.

“Hali hii ni tofauti na wapinzani wao Yanga, ambao wamekuwa na muendelezo wa kikosi chao kwa muda mrefu, wakifanya maboresho machache tu kila msimu,” ameongeza Hans Rafael.

Pia amezungumzia mwenendo wa usajili wa wachezaji waliosajiliwa msimu huu, akidai kuwa, bado ni mapema kusema kama usajili wa Simba umewalipa, kwani baadhi ya wachezaji waliosajiliwa dirisha la Januari bado wanajitafuta ndani ya kikosi.

“Hata hivyo, wachezaji kama Ancet Oura wameanza kuonesha ubora wao, huku Clatous Chama akiendelea kuwa injini ya ubunifu licha ya kuonekana kuelekea mwisho wa kiwango chake cha juu,” amesema Hans Rafael.

Hata hivyo amemzungumzia goli kipa mpya wa timu hiyo, Tanji Kassali akisema kuwa bado hajathibitisha ubora wake kutokana na makosa yanayoigharimu timu.

Pia amemsifu beki wa kati raia wa Afrika Kusini, Rushine De Reuck namna anavyoendelea kuonesha ubora wake na kuipambania Simba SC.

“Kwa ujumla, usajili wa timu hiyo unakadiriwa kuwa na mafanikio ya chini ya wastani,” ameongeza.

Sambamba na hilo, Hans Rafael amemtaja Mohammed Bajaber kuwa ni mchezaji aliyeshindwa kufikia matarajio ya Simba SC kutokana na majeraha ya mara kwa mara.

“Uwezo wake aliouonesha akiwa Nairobi City Stars na Kenya Police hajauonesha kwasababu muda mwingi yupo chumba cha hospitali,” ameongeza Hans Rafael.

Hans Rafael hakusita kuzungumzia changamoto ya marefa kuwa na makosa yanayojirudia, ambapo amesema kuwa wanapaswa kuendelea kuwajibishwa maana baadhi yao wamekuwa sehemu ya kuumiza timu nyingi kwenye ligi.

“Lazima mkazo uwepo, na heshima ya marefa iweze kurudi,” ameongeza Hans.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button