Waomba kuongezewa muda likizo ya uzazi

KATIKA kuhakikisha usalama wa afya kwa watoto waliozaliwa kabla ya muda(Watoto Njiti), Serikali imeombwa kuwaongezea muda wa likizo ya uzazi wanawake wanaojifungua watoto kabla ya muda wa kawaida wa miezi tisa.

Mwito huo umetolewa na Rais wa Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (Mewata), Dk Matilda Ngarina wakati akizungumza na gazeti hili kuhusiana na haki za wanawake hao ikiwa ni wiki hii ambapo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii inaanza kupokea maoni kuhusiana na haki ya wanawake hao.

Dk Matilda alisema kuwa mahitaji ya watoto njiti ni makubwa huku yakihitaji uangalizi wa karibu zaidi kutoka kwa mama zao hivyo kupewa likizo ya uzazi ya muda mrefu ni kitu cha msingi.

Alisema kuwa wanawake hao wanatakiwa kupewa likizo zaidi miezi mitatu tofauti na likizo inayotolewa kwa wanawake waliojifungua kwa muda unaotakiwa wa miezi tisa.

Alisema mwanamke aliyejifungua kabla ya muda wa miezi tisa inatakiwa likizo yake ya uzazi ianzie kuhesabiwa huo mwezi aliojifungua kisha ujumulishwe kwa miezi mitatu ya likizo yake.

Alisema:“yani kinachotakiwa kwa sasa ni kuhakikisha kuwa wanawake waliojifungua kabla ya muda wa miezi tisa inapaswa kwanza kuangalia huo mwezi aliojifungua ilikuwa imebakia miezi mingapi kufikia miezi tisa kisha aanze kupumzika kuanzia hapo,

Yani kama akizaliwa mimba ikiwa na miezi saba yani inakuwa ni bado miezi miwili kujifungua hivyo anatakiwa kuanza kwa kupewa miezi hiyo miwili kupumzika kisha ikimalizika apewe miezi yake mitatu kama kawaida.”

Akizungumzia kuhusiana na hali anayokuwa nayo mama mwenye mtoto njiti, Dk. Matilda amesema kuwa anakuwa na majukumu mengi ambayo anatakiwa yeye mwenyewe kuyatimiza kwa mtoto kuanzia namna ya kumhudumia ilia pate joto la mama, ale vizuri ili kilo zitimie kwa kuwa wanazaliwa wakiwa na kilo chache.

“Zipo kesi mbalimbali za wamama kuwapoteza watoto wao kutokana tu kuwa nao mbali yani mwanamke anakuwa amerejea kazini wakati bado mtoto anahitaji uwepo wa mama yake kwa ukaribu zaidi, hivyo inawezekana wakati mtoto anapitia kipindi kigumu mama yake anakuwa kazini na hapo ndipo zipo kesi za watoto kufariki kutokanana kukosa ukaribu stahiki kwa wamama wao” anasema Dk. Matilda.

Gazeti hili limezungumza na Mwanamama Khadija Yunge ambaye ni mkazi wa Dodoma, mtoto wake mwenye miaka 18 alizaliwa njiti, amebainisha kuwa ilimlazimu kuacha kazi ili amhudumie mtoto wake huyo kutokana kukosa muda wa kutosha wa likizo ya uzazi.

Alisema,” inatakiwa kuwe na muda wa kutosha wa kuwahudumia watoto njiti kwa kuwa muda wa miezi mitatu hautoshi kabisa yani hawa watoto wanakuwa na mahitaji mengi na tena kwa umakini wa hali ya juu ambao siyo rahisi kwa dada wa kazi kutekeleza.”

Habari Zifananazo

Back to top button