Wapewa mbinu kuongeza utalii wa mikutano

VIONGOZI wa vyama vya kitaaluma nchini wamepewa mbinu za namna ya kuongeza utalii wa mikutano, ambao ni sehemu ya uchumi wa diplomasia wenye kukuza tija katika nyanja mbalimbali.

Hayo yamesemwa na Balozi Mindi Kasiga leo  Dar es Salaam katika ufunguzi wa mafunzo hayo yanayoratibiwa na kumbi za mikutano za AICC na JNICC yakitolewa chini ya wakufunzi maalum kutoka Taasisi ya ya Afrika ya Chama cha Watendaji (AfSAE ) .

Balozi Kasiga amesema viongozi hao kupitia vyama vyao wanafundishwa namna wanavyoweza kupata zabuni, ili mikutano mbaluimbali kutoka nje ya nchi na hata katika kanda iweze kuja Tanzania ili kuleta tija katika uchumi wa nchi.

Advertisement

“Mafunzo haya ni ya pili kutolewa kwa viongozi hao kwa ajili ya taasisi na mashirika yasiyo ya serikali yakijihusisha na shughuli mbalimbali kimataifa kikanda na kidunia,” amesema.

Amesema viongozi hao wanafundishwa namna ya kukutana na wana jumuiya kwenye nchi mbalimbali duniani wakihusika katika mikutano ya pamoja, ili kuleta uelewa wa pamoja na hamasa katika yale yanayojadiliwa katika taasisi zao.

“Kwa kupokea hayo mafunzo kwa masuala ya utalii wa mikutano kupitia mashirika hayo kimataifa na kikanda itaweza kuleta na kuvutia uwekezaji na hata biashara mbalimbali nchini, ili kuifanya Tanzania ijulikane kimataifa na sehemu sahihi kwa ajili ya kufanya mikutano hiyo,” amesema Balozi Mindi na kuongeza kwa kutolea mfano mwaka jana Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa dunia wa kilimo na hata wa utalii ,ambao uliweza kuongeza uwekezaji na biashara nchini.

Amesema kupitia mafunzo hayo ni mwendelezo wa utalii wa mikutano, lakini ni diplomasia ya uchumi inayotekelezwa kwa diplomasia ya mikutano kuvutia utalii, uwekezaji na hata biashara.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa AfSAE, Jeffers Miruka amesema mafunzo hayo yanawaandaa sio Watanzania pekee pia katika nchi za Rwanda, Uganda na hata Kenya yakiwa na lengo la kuhakikisha viongozi hao wanakuwa wamejipanga kujua nini cha kufanya kuhakikisha mikutano mbalimbali ya kidunia inakuja nchini.

Amesema ni muhimu kwa viongozi hao kujua namna ya kushindana katika zabuni mbalimbali, ili kuwezesha mikutano iwe ya kikanda ama dunia kufanyika nchini ili kuongez autalii wa mikutano.