Sakata la ekari sita Arusha lachukua sura mpya

ARUSHA: SAKATA la mfanyabiashara wa nafaka mkoani Arusha, Phillemon Mollel maarufu ‘Monaban’ juu ya uhalali wa umiliki wa eneo la ekari 6 mtaa wa Engoshowash Kata ya Moshono katika jiji la Arusha limeingia sura mpya baada ya mfanyabiashara Eva Aminiel kuonesha nyaraka halali za umiliki wa eneo hilo.

Aminiel amemtaka ‘Monaban’ kuacha kuupotosha umma na kuomba huruma kwa jamii na serikali na kusema kuwa kufanya hivyo ni kosa. Amesema alinunuwa eneo hilo katika mnada wa hadhara uliosimamiwa na kuratibiwa na kampuni ya Cityland kwa niaba ya Benki ya CRDB.

Akizungumza kwa niaba ya Aminiel, Elibariki Mungure maarufu kwa jina la ‘Mojaa’ alisema mnada wa hadhara ulifanyika Julai 2 mwaka 2021 na walilipa Sh milioni 430 na kufanikiwa kupata nyaraka halali za serikali juu ya umiliki wa eneo hilo la ekari 6 baada ya kufanikiwa kuhamisha umiliki kutoka kwa monaban.

Mojaa alisema baada ya mnada huo kufanyika Monaban alikimbilia Mahakama Kuu kupinga kuuzwa eneo analodai ni mali yake lake lakini Jaji Dafina Ndumbaro Machi 2 mwaka huu alitupilia mbali kesi hiyo na kumpa ushindi Aminiel.

Alisema eneo hilo hakuna kanisa kama anavyodai bali kuna nyumba ndogo inayotumiwa na mafundi kuhifadhi vifaa vya ujenzi lakini ameudanganya umma na waandishi wake kuwa ndani ya nyumba hiyo ni kanisa kitu ambacho sio cha kweli hivyo alimwomba Monaban kupeleka nyaraka anazodai za umiliki wa eneo hilo kwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha Joseph Mkude kama alivyoagizwa na sio kwenda kwenye vyombo vya habari na kuupotosha umma.

Mojaa alisema kwa sasa ametii agizo la Mkuu wa wilaya la kusitisha ujenzi wa ukuta wa kuzungusha eneo lote la ekari sita na anasubiri kwa hamu kikao kati yake na Monaban kwa Mkuu wa wilaya kwani yeye atakwenda na nyaraka zote za uhalali wa umiliki wa eneo hilo na uongozi wa Benki ya CRDB nao utahudhuria kikao hicho.

Naye, Monaban akizungumzia hilo alisistiza kuwa yeye ni mmiliki halali wa eneo hilo lakini hakuwa na nyaraka zozote za zinazoonyesha kuwa yeye anamiliki eneo hilo na kudai kuwa nyaraka hizo ataziwasilisha kwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha Joseph Mkude na sio mtu mwingine yoyote na kuiomba serikali kumsaidia kwa hilo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button