“Wapewe elimu kabla ya kukopa”

SERIKALI imezitaka taasisi za fedha kutoa elimu kwa wakopaji ili wawe na uelewa kuhusu masharti ya mikopo, viwango vya riba, gharama za ziada, na athari za kutorejesha mkopo kwa wakati kabla ya kusaini mikataba husika.

Ofisa Sheria Mwandamizi, Idara ya Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Ramadhani Myonga, ameyasema hayo wakati wa mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa na Wizara ya Fedha na Taasisi zake kwa wananchi wa Halmashauri ya Buchosa, Wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza.

Alifafanua kuwa taasisi za fedha zinapaswa kutoa taarifa sahihi na mafunzo kwa wateja wao kabla ya kusaini mikataba ya mikopo ili kuhakikisha wanachukua uamuzi wa kukopa wakiwa na taarifa sahihi.

“Serikali inaendelea kuweka sera na miongozo inayolinda wakopaji dhidi ya unyonyaji wa kifedha na kuhakikisha upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa maendeleo ya kiuchumi”, alisema   Myonga.

Aliongeza kuwa kukiwa na uwazi katika utoaji mikopo na elimu ikatolewa vizuri kwa wakopaji kutapunguza unyonyaji wa kifedha na kutawasaidia wananchi kufanya maamuzi sahihi kwenye mikopo wanayoomba.

Kwa upande wake Ofisa Maendeleo ya Halmashauri ya Buchosa, Wilaya ya Sengerema, Mkoa wa Mwanza, Grace Machunda, aliwahamasisha wanavikundi mbalimbali nchini kusajili vikundi vyao ili kupata mikopo ya Serikali na kusaidiwa kisheria kutakapotokea changamoto kwenye vikundi.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo ya elimu ya fedha, mkazi wa Buchosa, Musa Kilaba, aliwashauri washiriki wenzake wa mafunzo hayo kwenda kufanyia kazi walichofundishwa.

Kilaba aliishauri Serikali kuongeza semina za mafunzo ya elimu hiyo katika ngazi zote nchini na kuongeza idadi wa watoa elimu ili waweze kuwafikia wananchi wengi kwa mara moja.

Naye Laurencia Msabi, mkazi wa Buchosa, aliahidi kuwa Balozi wa elimu ya fedha katika vikundi ambavyo ni mwanachama  na jamii inayomzunguka.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button