Wapiga kura Longido wajitokeza kwa wingi

JUMLA ya wapiga kura 79,768 waliojiandisha kupiga kura katika Jimbo la Longido mkoani Arusha wamejitokeza kwa vingi katika vituo vya kupiga kura lengo ni kutimiza wajibu wao wa kuwachagua viongozi wa vijiji na vitongoji katika Jimbo hilo.

Msimamizi wa uchaguzi katika Wilaya ya Longido na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Longido, Nassoro Senzigwa amesema wananchi wengi wamejitokeza kupiga kura katika vituo na ana uhakika hadi kufikia saa 9 mchana msululu wa watu utakuwa umepungua na kumalizika ndani ya muda uliopangwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za uchaguzi.

Senzigwa amesema kujitokeza kwa wingi kwa wananchi ni kutokana na elimu ya uchaguzi wa viongozi iliyowaingia wananchi hao ambao wengi wao ni wa jamii ya kifugaji katika maeneo mbalimbali ya kata 18 za jimbo hilo lenye vijiji 51 na vitongoji 176.

Advertisement

Amesema vyama vilivyojitokeza kuweka wagombea katika nafasi mbalimbali ni vyama vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambapo chama hicho kimeweka wagombea katika vijiji vyote na vitongoji, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeweka wagombea katika kijiji cha Namanga A na vitongoji sita vilivyopo katika Kata ya Namanga na Chama cha ACT Wazalendo kimeweka mgombea mmoja katika kijiji cha Longido Mjini tu.

‘’Hali ni shwari na watu wamejitokeza kwa wingi kupiga kura katika vituo 222 vya jimbo la Longido na sasa hivi niko katika kata za mpakani mwa Tanzania na Kenya nikiangalia upigaji kura ukiendelea,amesema Mkurugenzi wa Longido

Naye Mkuu wa Wilaya ya Longido, Salumu Kalli amesema pamoja na ugumu wa jiografia ya Jimbo la Longido hilo halikuwatatiza wananchi kwani wamejitokeza kwa wingi katika vituo vya kupiga kura lengo ni kutimiza wajibu wao wa kuchagua viongozi wa vijiji na vitongoji.

Kalli amesema katika kuhakikisha hali inakuwa salama yeye alikuwa katika Kata ya Kamwanga iliyoko mpakani wa Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro akikagua upigaji kura na kusisitiza kuwa elimu iliyotolewa na tume ya uchaguzi imewaingia wananchi wengi wa Jimbo la Longido.

‘’Nipo Kata ya Kamwanga mpakani wa Longido na wilaya ya Rombo wananchi wamejitokeza kwa wingi na foleni ni kubwa lakini hadi kufikia saa 10 jioni kila mmoja atakuwa ametimiza wajibu wa kumchagua kiongozi anayemtaka’’amesema Mkuu wa Wilaya

Naye Solomoni Lekui mkazi wa Kata ya Kimokouwa wilayani Longido amesema upigaji kura umepigwa kwa usalama mkubwa na wananchi wamekijitokeza kwa wingi katika Kata hiyo ili kumchagua kiongozi wanayempenda kwa maendeleo yao.

Lekui amesema msululu wa watu katika vituo unaweza kumalizika kwa wakati ukizingatia kuwa vituo vyote vilianza kupiga kura kwa muda uliopangwa wa saa 2 asubuhi na hiyo inaweza kusaidia wagombea waliochaguliwa kutangazwa ndani ya muda muafaka.

Naye Naibu Waziri wa Madini na Mbunge wa Jimbo la Longido,Dk Steven Kiruswa amesema amepiga kura kijiji kwake katika kijiji cha Olbomba mahali alipojiandikisha na amesema hali ni shwari kwani wananchi wamejitokeza kwa wingi kutimiza wajibu wa kuchagua viongozi wa vijiji na vitongiji wanaowaona wanafaa kuchaguliwa.