MAKAMU wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba amepongeza hatua za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukabili rushwa kwenye uchaguzi.
Alisema kwa kuwa vita dhidi ya rushwa si ya siku moja, CCM haina budi kuhakikisha mapambano ya kumshinda adui huyo yanakuwa endelevu kwa kusimamia misingi ya kuanzishwa kwa chama hicho.
Jaji Warioba amesema hayo wakati Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi alipomtembelea nyumbani kwake Dar es Salaam kwa ajili ya kumjulia hali.
“Hivi mlivyoanza ni safi, ‘in the long run’ (hatimaye huko mbele) tutakuwa na mwanga wa mapambano dhidi ya
rushwa. Nilikuwa na hamu kubwa kujua mabadiliko hayo kwenye Katiba ya chama, nilivyoshindwa kuwepo kwenye
Mkutano Mkuu Maalumu. Ni muhimu sana CCM iendelee kusimamia misingi yake ikiwemo ahadi za wanachama,”
alisema Jaji Warioba.
Aliongeza: “Vita hii si ya siku moja, ni muhimu muda wote chama kitafute njia za kuzuia rushwa kwa kusimamia misingi yake. Watu wazungumzie sifa na miiko ya uongozi. Wazungumzie sera, si hela. Kihistoria, CCM ni chama cha itikadi, sera na ilani. Kina wajibu wa kuonesha matumaini wapi tunawapeleka watu,” alisema.
Jaji Warioba pia, alisema vyama vya siasa vinapaswa kutofautiana kwa sera na dira ya namna ya kuwatumikia watu badala ya kutumia muda mwingi kuzungumzia namna ya kupata madaraka.
Wakati huo huo, mjane wa Baba wa Taifa, Julius Nyerere, mama Maria Nyerere ameitaka CCM iendelee kutimiza wajibu wake wa kuzisimamia serikali zake zote mbili ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na uwezo wa kujitegemea hasa katika kujilisha.
“Uhuru wa taifa unakamilika zaidi pale taifa linapojitegemea, hasa katika kujilisha na kuwa na chakula,” alisema alipozungumza na Dk Nchimbi.