Wasaidizi wa kisheria wafundwa

DODOMA: JUMLA ya wasaidizi wa kisheria 300 wanatarajiwa kupatiwa mafunzo maalum kuhusu sheria zilizopo, kanuni, miongozo, na sera zinazohusiana na utoaji wa msaada wa kisheria nchini.
Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wasaidizi hao, maarufu kama paralegals, ili waweze kuendelea kutoa elimu na huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi bila malipo, hususan katika maeneo ya pembezoni.
Kwa mujibu wa Wizara ya Katiba na Sheria, mafunzo hayo yatafanyika kwa awamu nne, ambapo awamu ya kwanza inahusisha washiriki 42 kutoka mikoa ya Arusha, Dodoma, Singida, Manyara, na Tanga. Mafunzo hayo yatadumu kwa siku 15.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo jijini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu Dkt. Franklin Rwezimul alisema serikali inaendelea kuboresha mifumo ya msaada wa kisheria kwa kuanzisha Madawati ya Msaada wa Kisheria katika halmashauri zote nchini.
“Lengo la serikali ni kuhakikisha kila kata inakuwa na msaidizi wa kisheria. Hadi sasa idadi yao bado ni ndogo, lakini jitihada zinaendelea ili kufanikisha azma hii,” alisema Dkt. Rwezimul.
SOMA:Kampeni msaada kisheria yarejesha matumaini Pwani

Alitoa wito kwa washiriki wa mafunzo hayo kutumia fursa hiyo kuimarisha ujuzi wao na kutoa huduma kwa wananchi kwa moyo wa kujitolea, hasa kwa makundi yenye uhitaji mkubwa wa msaada wa kisheria.
Aidha, aliitaka taasisi kushirikiana na Wizara katika kuwezesha wasaidizi wa kisheria kwa kuwajengea uwezo katika masuala mbalimbali ya kisheria. Pia, aliwataka kuandaa na kufanya Kongamano la Mwaka la Wasaidizi wa Kisheria, ambalo litakuwa fursa ya kujadiliana kuhusu changamoto na fursa wanazokutana nazo katika utoaji wa huduma za msaada wa kisheria nchini.
“Na hii ijumuishwe na wasaidizi wa kisheria waliojisajili kwa mujibu wa Sheria ya Msaada wa Kisheria Na. 1 ya Mwaka 2017 na Kanuni zake za Mwaka 2018,” aliongeza.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Legal Services Facility (LSF), Amani Manyelezi, alisema mfuko huo umekuwa ukiunga mkono msaada wa kisheria kwa zaidi ya miaka 12 kwa kushirikiana na mashirika 184 na wasaidizi wa kisheria zaidi ya 3,000 nchini.
“Tunalenga kuweka mazingira wezeshi kwa wasaidizi wa kisheria kwa kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria, huku tukizingatia usawa wa kijinsia na kupambana na ukatili wa kijinsia, hasa dhidi ya wanawake na watoto,” alisema Manyelezi.
Aliongeza kuwa kila mwaka wasaidizi wa kisheria wanawafikia zaidi ya wananchi milioni 6, wengi wao wakiwa wa maeneo ya vijijini ambako huduma za msaada wa kisheria ni adimu.
Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 59 ya kesi zinazowasilishwa kwa wasaidizi wa kisheria hutolewa na wanawake, huku asilimia 41 zikihusisha wanaume. Kesi nyingi zinahusiana na masuala ya ndoa na mgawanyo wa mali.
Akizungumza kwa niaba ya Msajili wa Watoa Huduma za Msaada wa Kisheria, Laurent Burilo-Mwakilfehi, alisema licha ya kuwepo kwa wasaidizi wa kisheria 2,205 waliosajiliwa, bado kuna upungufu mkubwa wa wataalamu hao, hususan vijijini.
“Huduma ya msaada wa kisheria ni bure, hivyo tunawasihi wasaidizi wa kisheria kufanya kazi kwa uzalendo na moyo wa kujitoa. Hii ni kazi ya kiuchungaji, malipo yake ni kuona haki inatendeka kwa jamii,” alisema Mwakilfehi.




