Wasanii kuwaenzi watu mashuhuri ‘Leaders’ kesho

WASANII wa Muziki, waigizaji, watangazaji na watu wengine mashuhuri wa tasnia mbalimbali nchini ambao walishafariki dunia watakumbukwa katika viwanja vya Leaders Club jijini Dar es Salaam kesho.

Akizungumza na HabariLEO kwenye maandalizi ya ibada ya kumbukizi hiyo, mratibu wa tukio hilo, Steven Mengere ‘Nyerere’ amesema tukio hilo litahusisha pia viongozi wa dini.

“Tarehe 7 Septemba 2024 kesho katika viwanja vya Leaders Club, tunakusanyika kwa pamoja kuwakumbuka na kuwaenzi wasanil/wadau wetu wapendwa ambao hawapo nasi tena,” amesema.

“Kwa kupitia sanaa na vipaji vyao, waliweza kugusa maisha yetu kwa namna ya kipekee na kuacha alama isiyofutika. Wasanii wa Tanzania, kwa umoja wao wanakukaribisha kuungana nao katika siku hii maalum ya kuwakumbuka, tukionesha heshima na upendo kwa wale walioacha urithi mkubwa katika tasnia yetu,”amesema Steve Nyerere.

Pia ameongeza kuwa kwa pamoja, wataendelea kuenzi michango hayo na kudumisha kumbukumbu zao katika mioyo yetu milele.’

Miongoni mwa wanaotarajia kuwepo ni pamoja na mchungaji Boniface Mwamposa, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo DamasNdumbaro pamoja na Naibu Waziri Wake Hamis Mwijuma Mwana FA pamoja na wengine wengi.

Habari Zifananazo

Back to top button