Watahiniwa kidato cha 6 waongezeka asilimia sita
DAR ES SALAAM; BARAZA la Mitihani la Taifa (NECTA) limetangaza kuwa watahiniwa 113,504 leo wanaanza mitihani ya kumaliza kidato cha sita huku wakiongezeka kwa asilimia sita ikilinganishwa na mwaka jana.
Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Said Mohamed alisema mitihani hiyo itafanyika hadi Mei 24, mwaka huu. Dk Mohamed aliwaeleza waandishi wa habari Dar es Salaam pia kuwa mitihani ya ualimu ngazi ya cheti na stashahada inaanza leo na kumalizika Mei 20, mwaka huu.
Dk Mohamed alisema mitihani ya kidato cha sita inafanywa katika shule za sekondari 931 na vituo vya watahiniwa wa kujitegemea 258 huku mitihani ya ualimu ikifanywa katika vyuo vya ualimu 99 nchini kote.
“Kati ya watahiniwa hao 113,504 waliosajiliwa wa shule ni 104,449 na watahiniwa wa kujitegemea ni 9,055 kwa idadi hii kuna ongezeko la watahiniwa kwa asilimia 6.19 ukilinganisha na watahiniwa wa mwaka jana waliokuwa 106,883,” alisema Dk Mohamed.
Alisema kati ya watahiniwa wa shule 104,449 wavulana ni 57,378 sawa na asilimia 54.9 na wasichana ni 47,071 sawa na asilimia 45.1 na kuwa watahiniwa wenye mahitaji maalumu ni 232 kati yao wenye uoni hafifu ni 201, wasioona 16 na wenye ulemavu wa viungo vya mwili ni 15.
Aidha, kwa watahiniwa wa kujitegemea waliosajiliwa ni 9,055 wavulana ni 5,515 sawa na asilimia 60.91 na wasichana ni 3,540 sawa na asilimia 39.09 na kuwa wenye mahitaji maalumu ni watatu ambao wote ni wenye uoni hafifu.
Dk Mohamed alisema kutoka watahiniwa 106,883 walisajiliwa mwaka jana mwaka huu idadi imeongezeka hadi kufika 113,504 ikiwa ni ongezeko la watahiniwa 6,621 sawa na asilimia 6.19 kwa mwaka 2024.
Alisema athari za mvua za El Nino zimeonekana mkoani Lindi na Shule ya Sekondari Kilwa ambayo imetoa taarifa kwa mamlaka husika ikiwemo Necta hivyo wanafunzi wa kidato cha sita watafanya mitihani katika Chuo cha Maendeleo (FDC-Kilwa).
Dk Mohamed alisema watahiniwa wa ualimu waliosajiliwa mwaka huu ni 11,552 na kati yao watahiniwa 2,766 ni wa ngazi ya stashahada na 8,786 ni wa ngazi ya cheti na kati yao wako wenye mahitaji maalumu ni 12.
Alisema mwaka jana watahiniwa waliosajiliwa walikuwa 8,479 hivyo kuna ongezeko la watahiniwa 3,073 sawa na asilimia 36.24 ya mwaka 2024 ukilinganisha na mwaka uliotangulia.
Dk Mohamed alisema maandalizi yamekamilika, mitihani imesambazwa kwenye vituo husika na nyaraka zote zinazohusu mitihani zimeshafika mikoa yote ya Bara na Zanzibar.
Necta imewaasa wasimamizi kuhakikisha watahiniwa wenye mahitaji maalumu wanafanya mitihani ipasavyo ili wapate haki yao ya msingi ikiwa ni pamoja na kuwapa mitihani yenye maandishi ya nukta nundu na kuongezewa muda wa mtihani kama ilivyoelekezwa.



