Wataka mfumo ustawi wa jamii kuangaliwa upya  

CHAMA cha ACT Wazalendo kimeishauri serikali kuangalia upya mfumo wa hifadhi ya jamii ili ndani yake uwe na bima ya afya itakayowezesha utoaji wa huduma za afya kwa Watanzania.

Wakizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, wasemaji wa sekta ya afya wa chama hicho, Ruqayya Nassir na Mwanaisha Mndeme ambaye ni Msemaji wa Sekta ya Uwekezaji, Mashirika ya Umma na Hifadhi ya Jamii, walitoa mapendekezo kwa serikali ambayo walisema yataboresha bima ya afya kwa wote.

Mndeme alisema kila mwananchi mwenye ajira rasmi na kukatwa michango ya Hifadhi ya Jamii ikiwemo NSSF na PSSSF ni vyema apate fao la matibabu ambapo mchango wa mwajiriwa wa 1/5 upelekwe kwenye bima ya afya.

Alisema kila mwananchi aliyejiajiri kwenye sekta ya kilimo, biashara au shughuli nyingine yeyote na ni mwanachama wa hiari katika mfuko wa hifadhi ya jamii anayechangia kiwango cha chini cha mchango wa mwezi cha Sh 30,000 achangiwe na serikali theluthi ya mchango kila mwezi.

“Hii itakuwa kivutio kwa watu walio kwenye sekta isiyo rasmi kujiunga kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii na kupata bima ya afya. Katika hili, Mfuko wa NSSF utapaswa uwasilishe 1/5 ya mchango kila mwezi kwa ajili ya fao la matibabu la mwanachama,” alisema Mndeme.

Alisema yeyote ambaye ni mnufaika wa TASAF, serikali itapaswa kumlipia mchango wake kwenye hifadhi ya jamii kwa asilimia 100 na kwamba mifuko ya hifadhi inapaswa kuanzisha fao maalumu la kuwawezesha wananchi hao kuzalisha kipato ili kufikia kundi la kuchangiwa theluthi.

Mndeme alisema Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) ndiyo itapaswa isimamie na kudhibiti Skimu ya Bima ya Afya badala ya Mamlaka ya usimamizi wa Bima (TIRA) kama ilivyo sasa.

“Kwa mapendekezo haya, tuna uhakika wa kila Mtanzania mwenye umri zaidi ya miaka 18 kuwa na bima ya afya kama fao miongoni mwa mafao ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii nchini,” alisema.

Nassir alisema kama serikali itakubali mapendekezo hayo itapaswa itenge kila mwaka katika bajeti yake asilimia 2.5 ya Pato la Taifa la mwaka uliotangulia kama fedha za kuchangia mfumo huo.

Pia alisema serikali haitakuwa tena na jukumu la kuendesha vituo vya kutoa huduma za afya kwani kwa mfumo huo vituo vitajiendesha vyenyewe na kwa ufanisi mkubwa.

“Uwezo wa nchi kuweka akiba utakuwa mkubwa na hivyo serikali kuwa na fursa ya kupata fedha za ndani kuwekeza kwenye miradi ya kimkakati itakayowezesha watu wengi zaidi kuwa kwenye ajira rasmi na hivyo kupunguza kundi kubwa la kuchangiwa,” alisema Nassir.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button