Wataka rais aendelee uteuzi NEC
DODOMA: WATOA maoni katika siku ya pili ya kuboresha miswada ya sheria nne zinazohusu uchaguzi wametaka Rais aendelee kuteua Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi.
Pia wamesema ni vema wakurugenzi waendelee kusimamia uchaguzi kama ilivyo kwenye sheria ya sasa.
Hayo ni baadhi ya maoni yaliyotolewa jana, ikiwa ni siku ya pili kwa wananchi kutoa maoni ya kuboresha miswada hiyo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria.
Mmoja wa watoa maoni, Mussa Mpanduchi alishauri kifungu cha sheria kinachotaka mwenyekiti na makamu wa tume kuteuliwa na rais kibaki kama kilivyo na kusisitiza kuwa rais ndio mwenye uzalendo namba moja na atateua watu wanaofaa kwa kuangalia sifa na weledi na kuwa akiteuliwa hawezi kutekeleza mamlaka ya uteuzi bali atatekeleza sheria za uchaguzi.
Naye Getrude Alphonce alisema wanaopinga wakurugenzi au watumishi wa umma kuteuliwa kusimamia uchaguzi ni hali ya kutoaminiana na kuwa hulka ya mtu isiharibu sifa ya taasisi nzima.
Amani Mulagizi alisema ibara ya 45 ya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Ubunge na Madiwani ibaki kama ilivyo ambapo washindi katika nafasi hizo wanaamuliwa kwa wingi wa kura.
“Ibara inayoelekeza rais anapatikanaje kibaki kama kilivyo, mwamko wa wananchi wetu katika kushiriki katika kupiga kura ni ndogo, hivyo tukisema tumpate kwa kupata kura zaidi ya asilimia 50 kutaifanya serikali kupata hasara kwani itakuwa ni ngumu kuifikia,” alisema.
Aidha, Mwenyekiti wa Kamati, Joseph Mhagama ameonya wachangiaji kuondoa hisia za kichama wakati wa kutoa maoni ya kuboresha miswada ya sheria.
Alisema pamoja na wabunge kutokana na vyama vya siasa lakini wawapo bungeni wanawakilisha wananchi na kuonya wale wanaochangia kwa hisia za vyama.
“Kuna watu wanahojiwa nje ya ukumbi na vyombo vya habari wakidai kuna haki ya kuzungumza imeminywa, sasa ni lazima tufuate taratibu za kutoa maoni na hakuna mtu maarufu kuliko Bunge, mtu akitaka kutafuta umaarufu atafute nje ya kikao hiki ambao anaweza kuendeleza uanaharakati.
Kamati hii kazi yake ni kupokea maoni ya kuboresha miswada yetu kwa mustakabali wa taifa letu,” alisema.
Akitoa maoni ya Jukwaa la Vijana Wachambuzi, Idi Mkazi, alishauri umri wa kugombea urais uwe miaka 35 badala ya 40 ya sasa huku kwa nafasi ya ubunge, diwani na kiongozi wa mamlaka ya serikali za mitaa iwe miaka 18.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Kanisa Katoliki la Dar es Salaam, Juda Thadeus Ruwa’ichi alishauri wajumbe wa tume ya uchaguzi wawe waadilifu na wenye elimu ya chuo kikuu.
Kwa upande wa asasi za kiraia, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Dk Ananiel Nkya alishauri kuwa marekebisho ya miswada ya sheria za uchaguzi yasiangalie vyama bali mustakabali wa nchi ili kuwa na umoja wa Watanzania wote.
“Kama tunalitakia mema taifa letu na kama Watanzania na wabunge tunawaomba tuangalie Tanzania kwa jicho tofauti, tufanye marekebisho bora, tusiangalie vyama vyetu maana vyama vinaweza kuwepo au visiwepo lakini tunachotaka kiwepo ni Tanzania yenye amani, heshima na umoja wa Watanzania wote,” alisema.
Pia alishauri Sheria ya Uchaguzi Rais, Wabunge na Madiwani kuongeza kifungu kipya ambacho kitaainisha mahitaji ya watu wenye ulemavu kwa kuwa na vifaa vya uchaguzi na miundombinu inayozingatia watu wenye mahitaji maalumu.
Dk Nkya pia ameshauri sheria ya uchaguzi kutoa wajibu kwa vyombo vya habari wakati wa uchaguzi kutoa fursa sawa za wagombea kueleza sera zao.
Pia kwenye kifungu kinachotaka ushirikishwaji wa makundi maalumu, amependekeza asilimia 30 itengewe kuwajengea uwezo vijana, watu wenye ulemavu na wanawake.
Maoni kutoka TLS imetaka Sheria ya Uchaguzi isomeke Sheria ya Taifa ya Uchaguzi ili iweze kusimamia chaguzi nyingi isiwe za urais, ubunge na madiwani pekee.
Pia imeshauri sheria iweke takwa la mdahalo kuanzia ngazi ya urais, ubunge na udiwani ili kuwafahamu wagombea na kuweka ukomo wa muda kutangaza matokeo.
Maoni kutoka Twaweza wametaka dosari ndogondogo ambazo zinaweza kurekebishwa zisiwe sababu za kumkosesha sifa ya kugombea isipokuwa zile za kikatiba.
Naye Suzan Lyimo wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) wameshauri kila mwaka kuwe na uboreshaji wa daftari la kudumu la mpigakura na kutaka tume kuwa na mfuko maalumu wa kuiendesha.