Watakiwa kuacha ufugaji wa kizamani

KATAVI; Wafugaji mkoani Katavi wametakiwa kuachana na ufugaji wa kizamani wa kuhamahama na mifugo, badala yake wafuge kwa kuzingatia mbinu za kisasa za ufugaji zenye tija.
Wito huo umetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko kwenye kikao cha wadau wa sekta ya mifugo kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa mjini Mpanda.

Mrindoko amesema kumekuwa na migogoro baina ya wafugaji na wakulima, ambayo kwa kiasi kikubwa inasababishwa na wakulima kuhamahama na mifugo yao, hivyo kama zitatumika mbinu za kisasa kutakomesha migogoro hiyo.
Ameziagiza halmashauri zote za Mkoa wa Katavi kuhakikisha zinatengeneza mazingira wezeshi kwa wafugaji ikiwemo kutoa elimu kuhusu mbegu bora, madawa na chanjo za mifugo yao.
Kwa upande wao baadhi ya wawakilishi wa wafugaji waliohudhuria kikao hicho wameiomba serikali kuendelea kutoa elimu zaidi kuhusu nyanda maalum za malisho zilizotengwa na serikali, kwani kuna baadhi ya watu wasio na nia njema wameanza kuvamia na kuanzisha shughuli zingine tofauti na lengo la ufugaji.
Kikao hicho kimehudhuriwa na wadau mbalimbali wa mifugo wakiwemo wakuu wa Wilaya za Mpanda na Tanganyika, wazalishaji wa madawa na chanjo za mifugo, wasindikaji wa mazao ya mifugo na viongozi wa chama cha wafugaji.



