Watakiwa kujenga utamaduni kuweka akiba

WANANCHI wametakiwa kujengea utamaduni wa kujiwekea akiba ya fedha, ili ziweze kuwasaidia kwa maisha ya baadae.

Mwezeshaji kutoka Taasisi ya Dhamana ya Uwekezaji na Usimamizi wa Rasilimali Tanzania (UTT-AMIS), Grace Ngailo, ameyasema hayo wakati akitoa mafunzo juu ya uelewa na ujuzi kwenye masuala ya kifedha katika semina ya jinsia na maendeleo iliyoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) na kushirikisha makundi mbalimbali ya kijamii Dar es Salaam.

“Unaweza kuweka bajeti kwenye kile kipato unachopata, kwamba basi jitahidi kuweka asilimia kumi, ukiweza hata asilimia 20 kwa ajili ya akiba.

“Tunasema jilipe kwanza, ukiweza kujilipa kwanza na kujipa uthamani wewe na kuangalia uhuru wa kifedha ambao unatakiwa kuupata kwa baadae au kesho yako basi unaweza kuamua kujiwekea malengo, sasa hivi na ukaweza kuweka akiba,”  alisema.

Ngailo alisema kuwa utamaduni wa kuweka akiba humsaidia mtu, pale endapo atapatwa na dharura, lakini vilevile kujiwekea usalama wa kipato cha mwananchi kwa maisha yake ya baadae, mathalani kwa mfanyabiashara mdogo ambaye ikitokea akaumwa hana mahali kwingine kwa kumpatia kipato chochote.

Amesema kuwa uwekezaji kupitia UTT-AMIS kutawasaidia wananchi hao hususan wenye kipato cha chini kuweza kuishi vizuri, kutokana na kujiwekea akiba ambayo inampatia faida.

“Kwa hiyo sisi tunashauri kabisa kuwa wafanyabiashara wadogo watumie fursa ya UTT-AMIS waweke akiba, ili waweze kujipatia mahitaji yao mbalimbali.

“Tunasema uwekezaji unaweza kuanzia Sh 10,000 kwa mfuko wa umoja, Sh 5,000 kwa mfuko wa jikimu, lakini kwa wale wanaojiweza kuna mfuko unaitwa ukwasi ambao unawafaa sana wafanyabiashara kwa sababu unampa mtu uwezo wa kutoa pesa yake ndani ya siku tatu bila ya masharti yoyote,” alisema.

Mratibu wa mafunzo katika Idara ya mafunzo na uwezeshaji kutoka TGNP, Anna Sangai, anasema kuwa licha ya serikali kuweka juhudi kuwasaidia wanawake kujikwamua kiuchumi, bado wanawake hao wanakabiliwa na changamoto za mitaji kwa asilimia ndogo, ambazo huenda kwenye vikundi vya wanawake hao, hivyo kuiomba serikali kuangalia upya utaratibu wa ugawaji wa fedha hizo kwa wanawake hao.

Habari Zifananazo

Back to top button