Watakiwa kujitenga na ‘No Reform No Election’

GEITA: CHAMA Cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kimewatoa hofu wanachama wake waliojitokeza kutia nia na kugombea nafasi mbalimbali kamwe wasijiingize kwenye kampeni ya ‘No Reform No Election’.

Aidha Chaumma imewahakikishia watia nia watakaopitishwa kugombea nafasi mbalimbali kutokuwa na hofu kwani Chaumma imeweka mipango thabiti siyo tu ya kushiriki uchaguzi bali kuchukua mamlaka nchini.

Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Habari na Taarifa kwa Umma wa Chaumma, John Mrema ametoa kauli hiyo katika mkutano maalum wa kuzungumza na kukabidhi fomu watia nia udiwani jimbo la Geita mjini.

Amesema kamwe Chaumma haitakimbia uchaguzi kwa kuwa kususia uchaguzi pekee siyo njia ya kuzuia mabadiliko na hivo kujiweka kando kutakipa nafasi Chama Tawala kutunga sheria kwa matakwa yake.

“Tumeshiriki chaguzi tangu mwaka 1995 hapakuwa na reform, sheria zilikuwa hizo hizo, wasimamizi walikuwa haohao, lakini tuliwahi kufikisha wabunge wa upinzani 112 kwenye taifa hili.

“Sasa mtu akikwambia tunaenda kuzuia uchaguzi, huo muujiza haujawahi kutokea popte duniani, kama wanabisha waulizeni wawape nchi moja ya mfano ili tukaifanye iwe shamba darasa”, amesema Mrema.

Ameongeza pia Chaumma haioni haja ya kususia uchaguzi kwani ni kuwanyima wananchi haki wenye kiuu ya kuona mabadiliko ya sera, kanuni na sheria za nchi ili kufikia mageuzi makubwa ya kiuchumi nchini.

“Wananchi wetu wameshateseka sana, tunataka leo tukawaambie tena rudini kwenye mateso miaka mingine mitano, harafu miaka hiyo mitano mtarudi mikawaambie nini”, amesema Mrema.

Aidha Mrema amesisitiza kuwa ilani ya Chaumma katika uchaguzi mkuu 2025 ipo mbioni kukamilika na imelenga kuja na jawabu la moja kwa moja juu ya changamoto za kijamii na kiuchumi kwa kila watanzania

“Sisi Chaumma hatuendi kujibu umasikini wa jumla, tunataka kujibu umasikini wa kipato cha mtu mmoja mmoja, kwa sababu tukisema tutibu umasikini wa jumla wapo watu tunawaacha”, amesema.

Mrema ameeleza kuwa Chaumma kimeandaa mgombea urais mwenye uzoefu wa kisiasa na ushawishi mkubwa nchini ambaye atasaidia kueneza ilani ya chama na kuleta ushindani wa kweli katika uchaguzi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button