Watakiwa kutunza mazingira soko la samaki Mikindani
WAFANYABIASHARA samaki katika soko la feri lililopo Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara wametakiwa kutunza mazingira ili kuepukana na magonjwa mbalimbali ya milipuko yanayotokana na uchafu.
Elimu hiyo imetolewa wakati wa zoezi la ufanyaji usafi katika soko hilo la feri lililoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mtwara (MTPC) kwa kushirikiana na ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa hiyo pamoja na wadau wengine.
Akitoa elimu kuhusu masuala mbalimbali ya utunzaji wa mazingira kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Manispaa hiyo, Angelina Januari ambaye ni ofisa afya wa manispaa hiyo amesema wafanyabiashara wa sokoni hapo wanao wajibu wa kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa hayo.
Hata hivyo wahakikishe mazingira wanayofanyia shughuli zao yanakuwa safi wakati wote ili kulinda afya zao na za watumiaji wa soko hilo kwa ujumla ambapo moja ya magonjwa hayo ya milipuko ikiwa ni pomoja na kuhara, homa ya matumbo na mengine.
Ofisa Mazingira kutoka Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Maguri Wambura amewataka wafanyabiashara wa samaki sokoni hapo kukaanga samaki kwa kutumia nishati safi ili kulinda afya zao pamoja na mazingira yanayowazunguka
Kwa upande wake Katibu wa MTPC, Bryson Mshana amesema kutokana na muingiliano wa watu uliopo eneo hilo la feri wameona ni vyema kutumia eneo hilo kwa kufanya usafi pamoja na kutoa elimu ya magonjwa ya mlipuko kwa wananchi wanaofanya shughuli zao sikoni hapo.
Meya wa Manispaa hiyo, Shadida Ndile “Niwaombe wafanyabishara wote mnaofanya biashara katika soko hili la feri muendelee kufanya usafi na muufanye usafi kuwa utamaduni wenu wa kila siku kutokana na wingi wa watu uliopo katika eneo hili Kwa kuwa samaki ni chakula lazima auzwe katika mazingira safi”amesisitiza