Watalii kutoka Denmark wajinafasi ofisi za TSN Mwanza

MWANZA; Watalii kutoka nchini Denmark wako jijini Mwanza, Tanzania, kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii wilayani Ukerewe.

Kabla ya kuelekea Ukerewe leo Oktoba 17, 2023, wametembelea Kampuni ya magazeti ya Serikali (TSN), wakaeleza kwamba kikubwa kilichowavutia kutembelea Tanzania ni ukarimu wa Watanzania na wingi wa vivutio vya utalii.

“Ukarimu ndio kitu cha kwanza tunachotarajia kukutana nacho,” amesema mkuu wa msafara wa watalii hao sita, Joan Skriver Larsen.

Advertisement

Pamoja na vivutio vya utalii wilayani Ukerewe, watalii hao watatembelea kituo cha kulelea watoto wenye ulemavu wa ngozi na kutoa msaada wa miwani takribani 150 ya kuzuia makali ya mionzi ya jua kwa watoto hao.

“Tutatembelea pia kituo cha kulelea watoto yatima na kutoa msaada wa vifaa mbalimbali vya darasani kwa ajili ya kuandikia na kuchora, na vya michezo kwa watoto wadogo,” amesema.

Kwa upande wa vivutio vya utalii, wageni hao walioingia Mwanza juzi Oktoba 15 na kutarajia kukaa hadi mwisho wa mwezi huu, watatembelea jiwe linalocheza, hekalu la mfalme wa wakerewe, Gabriel Ruhumbika, pamoja na eneo la Kagungunri ambalo ni ngome ya kwanza ya Wamisionari.

Mmiliki wa Ufukwe wa Yamuyebe ambaye ndiye mwenyeji wao, Chrispine Mugimba, amesema watalii watajionea pia kiwanda cha kwanza wilayani ukerewe cha kuchakata zao la pamba , kilichoanzishwa mwaka 1905.

“Vilevile watafika kwenye pango lililotumika kama benki ya kuhifadhia fedha enzi hizo. Historia inasema wananchi walikuwa wakipeleka fedha zao kwa mfalme, ambaye aliwatuma watumishi wake kuzipeleka kwenye pango kuzihifadhi, hadi mwenye nazo alipopozihitaji.

“Wageni wetu watafika na kwenye shamba la miti Rubya, waone mnara mrefu ambao walinzi wa kijerumani walitumia kwa sababu za kuisalama. Ratiba yao hapa nchini ni kutembelea Ukerewe tu,” amesema.

2 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *