Watalii kutoka Qatar kupanda mlima Kilimanjaro

DAR ES SALAAM: Jopo la watalii kutoka Al Wakra Qatar Academy ya nchini Qatar limewasili Tanzania kwa safari yao ya kitaaluma inayoambatana na kupanda Mlima Kilimanjaro.

Ujumbe huo unajumuisha Mlezi wa Wanafunzi, Abdirahman Hussien Handule, wanafunzi sita, mwalimu mmoja na mzazi mmoja kama mwakilishi.

“Safari hii ya ajabu ni sehemu ya dhamira pana ya chuo kwa elimu ya nje, ukuzaji wa uongozi na ushirikiano wa kitamaduni,”

“Ni mwendelezo wa ushirikiano uliofanikiwa kati ya Ubalozi wa Tanzania mjini Doha na Al Wakra Qatar Academy, ambapo hadi sasa tayari tumefanya safari mbili kama hizi hapa Tanzania,” amesema kiongozi wa jopo hilo, Handule.

Mara baada ya kuwasili uwanja wa ndege wa KIA, jopo hilo lilipokelewa na Godwill Kyegeko, Ofisa Mwandamizi wa Utumishi wa Nje kutoka Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania.

Kuanzia leo Juni 16 hadi Juni 25, 2025, wanatazamiwa kupanda Mlima Kilimanjaro na kufanya ziara zilizopangwa katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, kijiji cha utamaduni cha Masai Boma, Maporomoko ya Maji ya Materuni na mashamba ya Kahawa mkoani Kilimanjaro.

Kama sehemu ya dhamira yao ya ushirikishwaji wa jamii, jopo hilo pia litatembelea Shule ya msingi ya serikali katika Wilaya ya Moshi Vijijini, ambapo watashiriki katika mazungumzo na jamii na wanafunzi, walimu na wasimamizi wengine wa shule.

Kwa mujibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Tanzania imeendelea kufungua milango ya watalii wakiwemo wanataaluma mbalimbali ili kuhakikisha dhamira ya serikali kuendelea kushuhudia watalii milioni 5 kila mwaka, inakuwa endelevu kwa miaka mingi ijayo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button