MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kagera imewafikisha mahakamani wafanyabiashara watano na kuwafungulia mashtaka tisa ya uhujumu uchumi ikiwemo kukwepa kulipa kodi.
Kodi hiyo inaelezwa ni kiasi cha zaidi ya Sh milioni 10. Shtaka lingine ni kutengeneza pombe kali bila kuwa na leseni.
Washtakiwa hao wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Bukoba, Janeth Masesa na kusomewa mashtaka yanayowakabili ambayo waliyatenda kwa kipindi cha mwezi Desemba mwaka 2024 hadi Februari 2025.
Kesi ya kwanza ni kesi namba 7238 ya mwaka 2025 inayowakabili washtakiwa wanne ambao ni Mwesiga Reopard, Nelius Kaizilege, Julieth Ishengoma na Herieth Gervas walioisababishia TRA hasara ya zaidi ya Sh milioni 10.
Kesi ya pili ni kesi namba 7243 ya mwaka 2025 inayomkabili mshtakiwa mmoja Mulokozi Egbert (39) anayekabiliwa na mashtaka nane ambapo aliisababishia hasara Mamlaka ya TRA zaidi ya Sh milioni 1.
Baadhi ya mashtaka mengine yanayowakabili ni pamoja na kushindwa kuomba kibali cha kutengeneza bidhaa zenye ushuru kwa ajili ya eneo la utengenezaji na utunzaji, kushindwa kuwasilisha marejeo ya bidhaa zenye ushuru zilizozalishwa, kushindwa kutunza kumbukumbu za stempu za kielektroniki na kusaidia ukwepaji kodi ya ushuru wa bidhaa
Hata hivyo washtakiwa wote wamekana mashtaka hayo na kupata dhamana baada ya kutimiza vigezo
Kwa upande wa Jamhuri kesi hiyo inasimamiwa na mawakili wa serikali ambao ni Judith Mwakyusa, Grolia Lugeye na Alex Giryago huku kwa upande wa utetezi ni wakili Projestus Mulokozi na Frank Kaloli.
Kesi ya kwanza inayowakabili washtakiwa wanne itaendelea tena April nane huku kesi ya pili itaendelea tena Aprili mbili mwaka huu.