Watano washinda Malkia wa Nguvu Kusini

WASHINDI watano wa tuzo za Malkia wa Nguvu Kanda ya Kusini wamekabidhiwa tuzo zao usiku wa Agosti 25 katika ukumbi wa Police Officers Mess.

Tuzo hizo zimejumuisha washiriki kutoka Ruvuma, Lindi na Mtwara.

Advertisement

Washindi hao ni mwanamke mwenye ushawishi tuzo aliyopewa Mwanaidi Sexbeti Mdendemi ambaye alipitia ubaguzi na manyanyaso baada ya mume wake kufariki, hakupata mali, aliachiwa watoto watatu, maisha yaliharibika, akawa mlevi, lakini alifanikiwa kuanza maisha upya kwa kuuza mandazi kwenye beseni na sasa amekuwa mjasiriamali mwenye ushawishi sana Mtwara.

Tuzo ya biashara ya chakula imeenda kwa Paulina Maivaji maarufu kama MC Pau, mwalimu wa shule ya msingi, alianza biashara ya chakula kama mpika chipsi wilayani Tandahimba, kwa sasa biashara yake imekua kubwa, amekua na uwezo kulisha sherehe tano mfulululizo na kwa pamoja.

Upande wa biashara ya mapambo mshindi ni Martha Francis Chiwango Mkurugenzi wa Martha Decorations yeye ni mfanyabiashra aliejikita katika upambaji, alianza safari yake ya mapambo kwa kujitolea kupamba kanisani na kwenye maharusi, baadaye akaanza kulipwa kwenye kazi hizo, sasa ndie mpambaji namba moja Lindi na Mtwara.

Tuzo ya mjasiriamali bora mshindi ni Subira Kabula maarufu kama mama Sasuria, mmiliki wa shule za Sasuria Day Care and Primary Schools. Sababu ya kuanzisha ‘day care’ ni baada ya kupata changamoto ya kumlea mtoto akaamua aanzishe sehemu ya kulelea watoto ambapo ndiyo hiivi leo inaitwa Sasurea Day Care and Primary Schools.

Fidea Bright Ausi amekua Malkia wa Nguvu kwenye kipengele cha Ustawi wa Jamii, yeye ni binti kutoka Mtwara ambaye akiwa mdogo, ameanzisha taasisi yake ya FB Empowerment nia na lengo ni kuwasaidia mabinti wa mikoa ya kusini kupata nafasi katika  nyanja mbalimbali za kiuchumi.

Mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma (Mwana FA) amewataka Malkia wa Nguvu kuwa sehemu ya mabadiliko chanya kwenye sehemu wanazoongoza akitoa mfano wa Rais Samia Suluhu Hassan namna alivyobadilisha mwelekeo wa  nchi kibusara, ujasiri na maono makubwa.