Watanzania tusaidie chakula kwa majirani EAC, lakini…

Rais Samia Suluhu Hassan

RAIS Samia Suluhu Hassan, Jumapili aliwaondoa wasiwasi na kuwathibitishia Watanzania kuwa, bado Tanzania ina chakula cha kutosha na hakuna tishio lolote la kuwa na njaa.

Alibainisha hayo wakati akizungumza katika kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya Miaka 50 ya Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) Dar es Salaam alipoweka wazi kuwa, katika ghala la hifadhi ya taifa ya chakula, kuna takribani tani 150,000 za chakula kinachoweza kutumika endapo kutatokea wakati mgumu wa upungufu wa chakula.

Ninampongeza na kumshukuru Rais Samia kwa kuweka bayana ukweli huo uliowaondolea hofu Watanzania mintarafu upungufu wa chakula.

Advertisement

Ufafanuzi wa Rais Samia umekuja pia siku chache baada ya serikali kupitia Wizara ya Kilimo kutangaza kuwa, haijasitisha utoaji wa vibali vya kusafirisha mazao ya chakula nje ya nchi kama ilivyokuwa imeripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Wizara kwa kufuata taratibu zote za kisheria, inaendelea kutoa vibali vya kusafirisha mazao ya chakula kwenda nje ya nchi jirani zikiwamo nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kupitia mfumo wa utoaji vibali wa kielektroniki.

Katika kipindi cha kuanzia Agosti 27 hadi Septemba 7, mwaka huu wizara imetoa vibali vya mahindi, maharage, unga na mchele kwenda nje ya nchi vyenye jumla ya tani 37,450.

Ninawapongeza pia Watanzania hasa Serikali kwa kuruhusu na kuendeleza utoaji wa vibali hivi ili kuwasaidia wananchi wa EAC ambao kwa sababu moja ama nyingine zikiwamo za mabadiliko ya tabianchi na Covid-19, walishindwa kuzalisha na kupata chakula cha kutosha.

Ninaipongeza serikali kwani isingekuwa imetenda vema na najua isingeweza kufanya hivyo, eti ikasimama na kukumbatia chakula kingi huku ndugu na majirani wakifa kwa njaa.

Hii inatokana na ukweli kuwa, jirani yako ndiye nduguyo na ni kwa msingi huo, ninazidi kuiunga mkono serikali kwa kuendelea kuruhusu uuzaji wa mazao hasa ya chakula kwa vibali vinavyotolewa kwa umakini.

Hata hivyo, nionavyo mimi, utoaji vibali uende sambamba na ongezeko la nguvu za kudhibiti ‘njia za panya’ na biashara ya chakula kwa njia ya magendo kwani hili linaweza kusababisha upungufu wa chakula.

Biashara na usafirishaji holela wa chakula kwenda nje ya nchi usiachwe kuendelea kwani unaweza pia kusababisha kukua kwa bei ya vyakula kama mahindi, mchele na vingine kama inavyoonekana sasa katika masoko na maduka mbalimbali na kusababisha vilio.

Ndio maana ninasema, Watanzania tuwasaidie chakula kwa majirani EAC ili wasife wala kuteseka kwa njaa, lakini tuwe makini dhidi ya magendo na ulanguzi katika mashamba hasa katika mikoa ya mipakani ili kuepuka njaa na kudhibiti bei.