Watanzania wako tayari kumchagua Samia

TABORA : MSANII wa vichekesho nchini, Kingwendu, amepongeza hamasa kubwa ya wananchi kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29 mwaka huu, akisema Watanzania wako tayari kumchagua tena Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na maendeleo makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha uongozi wake.
Akizungumza baada ya kushiriki mkutano wa kampeni wa mgombea mwenza wa urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, uliofanyika katika Uwanja wa Kigwa B, Jimbo la Igalula, Wilaya ya Uyui mkoani Tabora, Kingwendu alisema wananchi wameona kazi kubwa iliyofanywa na Rais Samia ndani ya muda mfupi, ikiwemo utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.
SOMA: Kairuki aahidi kujenga barabara tisa Goba
Amesema mafanikio hayo yameongeza imani kubwa kwa wananchi kumchagua tena Rais Samia ili aendelee kuongoza taifa kwa awamu nyingine. “Watanzania wameona kazi kubwa iliyofanywa na Rais Samia, kuanzia miradi ya elimu, afya, barabara, maji na uwezeshaji wananchi kiuchumi. Imani kwa uongozi wake imeongezeka kwa kiwango kikubwa,” alisema Kingwendu.
Aidha, amewataka Watanzania wote kujitokeza kwa amani na wingi siku ya kupiga kura Oktoba 29, 2025, ili kutumia haki yao ya kidemokrasia kuchagua viongozi wanaoleta maendeleo.



