Watanzania washauriwa kuandika wosia kuepuka migogoro

KATIBU Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria, Mary Makondo

DAR ES SALAAM: KATIBU Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria, Mary Makondo ametoa wito kwa Watanzania kuandika wosia ili kupunguza migogoro kwenye familia pindi wanapofariki dunia.

Akizungumza na HabariLEO jana alisema Kampeni ya Msaada wa Kisheria wa Mama Samia (MSLAC) imekuwa ikipokea malalamiko mengi ya mirathi.

“Pale wapendwa wetu wameondoka hapa duniani na wameacha mali wanatakiwa wawe wameandika ili kujua nani atasimamia na pale msimamizi anaposimamia na hafanyi vizuri kuna nafasi ya kutumika mahakamani na kuondolewa,” alisema.

Advertisement

Alisema MSLAC inawasaidia watu namna ya kuandika wosia na jinsi ya kuuhifadhi.

“Tutawasaidia namna gani wosia unapaswa kuandikwa ili atakayesimamia asimamie na kufuata taratibu za kimahakama ili mwisho wa siku kusiwepo na migogoro katika jamii,” alisisitiza.

Alisisitiza migogoro mingi inatokana na mirathi na ardhi ambayo kila Mtanzania anayo haki kumiliki ardhi.

Makondo alisema kampeni hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine wataendelea na utoaji elimu na kutatua kero za wananchi katika suala la haki na kuongeza kuwa serikali imewawezesha bajeti ili kufikia mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar ambapo mpaka sasa mikoa saba imekwishafikiwa.

Alisema huduma zinazotolewa kwa wananchi ni pamoja na haki za wafungwa, haki za watoto na haki za walioko vizuizini. Naye mkazi wa Dar es Salaam, Yunus Lingani alisema kampeni hiyo imemsaidia kupata haki yake.

Soma hapa: Makanjanja kaeni chonjo msaada wa sheria wa Samia

“Nilikuwa na viwanja viwili maeneo ya Mkuranga nikadhulumiwa tangu mwaka 2009, nilianza kufuatilia mpaka mwaka jana ndio nikapata haki ya umiliki wa kiwanja kimoja na kingine bado naendelea kufuatilia,” alisema.

Akizungumzia suala hilo la Lingani, Makondo alisema japo shauri la kiwanja kimoja limemalizika bado kuna kazi ya kufanya ikiwemo kujaza hukumu.

“Huyu mwananchi tutaendelea kumsimamia ikiwa ni pamoja na kukazia hukumu ili jambo likamilike,” alisema.

Soma hapa: Msaada wa kisheria kwa wanyonge waja

/* */