Watatu wafariki dunia ajali ya ndege Bukoba

WATU watatu waliokuwa kwenye ndege ya Precision Air iliyotumbukia Ziwa Victoria ilipokuwa ikikaribia uwanja wa ndege wa Bukoka wamefariki dunia, afisa mwandamizi wa serikali amewaambia waandishi wa habari.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera (RMO) Dk. Issessanda Kaniki amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo baada ya zoezi la uokoaji lililoendelea kwa saa kadhaa na kuokoa watu 26 kati ya 43.
Rais Samia Suluhu Hassan alituma salamu za faraja kwa familia na kutoa wito wa utulivu. Waziri Mkuu amepanga kutembelea eneo hilo ili kuimarisha kazi ya uokoaji.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Precision Air Bw. Patrick Mwanri alielezea ajali hiyo kama “janga” akitangaza vituo viwili vya habari vya Dar es Salaam na Bukoba.
Kwa mujibu wa maelezo rasmi, ndege hiyo ya abiria PW494 ilikuwa na abiria 39 na mtoto mchanga. Ndege hiyo ilitoka Dar es Salaam na ilipangwa kutua katika Uwanja wa Ndege wa Bukoba na kuelekea Mwanza kabla ya kurejea Dar es Salaam Jumapili.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Abert Chalamila amesema shughuli za uokoaji zinaendelea na vifaa vya kusaidia kutoka mkoani Geita na Kiwanda cha Sukari cha Kagera.