Wateja wapya Tanesco kukopeshwa majiko

SERIKALI imeliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) liharakishe mchakato wa kuwakopesha wateja wapya majiko ya umeme.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Dotto Biteko ametoa agizo hilo wakati wa uzinduzi wa programu ya utoaji majiko ya umeme kwa bei ya ruzuku kwa wafanyakazi 11,000 wa Tanesco.
“Tunapokwenda, wateja watapatiwa majiko yanayotumia nishati ya umeme wakati wa kuunganishiwa na watalipa kidogo kidogo kwa kipindi fulani ili tuwe na Watanzania wengi wanaotumia nishati hiyo kwenye kupikia,” alisema Dk Biteko.
Alisema matumizi nishati safi ya kupikia yana lengo la kupunguza athari za kiafya na kiuchumi zinazotokana na matumizi ya nishati zisizo safi na hivyo kuathiri afya za watu.
Dk Biteko alisema Watanzania hawana sababu ya kuogopa kutumia nishati ya umeme kwenye kupikia kwa kuwa gharama yake ni nafuu.
Kwa mujibu wa Dk Biteko takwimu zinaonesha ni asilimia 4.5 tu ya Watanzania wanatumia nishati ya umeme kupikia idadi ambayo ni ndogo kulingana na idadi ya Watanzania.
“Tafiti zinaonesha kuwa majiko janja ya umeme yanaweza kutumia chini ya uniti moja ya umeme sawa na Shilingi 352 kuandaa mlo moja, ukipika kwa majiko janga mlo moja kama ungetumia mkaa kile kikopo ungenunua Shilingi 2,000 lakini kwenye umeme haizidi Shilingi 500,” alisema.
Aliongeza: “Kila mfanyakazi wa Tanesco aone aibu kuwa na kuni au mkaa nyumbani kwake kwa ajili ya kupikia, aone fahari ya kutumia umeme ili unapowaambia watu wengine wewe uwe mfano wa kuyaishi yale unayoyazungumza”.
Alisema Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akitamani kuona Watanzania wengi wanatumia nishati safi kupikia.
Alizitaka taasisi nyingine kuiga mfano huo katika kuwapatia majiko ya ruzuku wafanyakazi wao ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga alisema utoaji wa majiko hayo ni utekelezaji wa mkakati wa nishati safi ya kupikia.
“Hii inaonesha tumeweza kuibeba ajenda ya nishati kwa vitendo ili wengine wakiona itakuwa vizuri kwani tumeamua kuwa vinara kwenye utekelezaji,”alisema Kapinga.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Lazaro Twange alisema Tanesco itaisaidia Tanzania kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ifikapo 2034.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi Tanesco, Balozi Zuhura Bundala alisema kutolewa kwa majiko hayo kwa watumishi wa Tanesco kutasaidia kuhamasisha wananchi kutumia majiko ya umeme.