Watendaji warahisishe huduma kwa wananchi, wasiwe vikwazo

AKIWA ziarani mkoani Njombe mwezi uliopita, Rais Samia Suluhu Hassan aliwataka viongozi wanaopewa dhamana ya kuhudumia wananchi wazingatie utawala bora na kuelekeza juhudi na akili zao katika kuhudumia wananchi badala ya kujifanya watawala.

Rais Samia anasema suala la utawala bora, viongozi wa ngazi za mikoa na wilaya na wale wa ngazi za chini, ni wahudumu wa wananchi.

Kwa mujibu wake, wananchi wanachotaka ni kusikilizwa hivyo viongozi wenye dhamana popote walipo wanapaswa kufanya hivyo na kuwatatulia shida zao pale wanapoona inafaa kufanya hivyo.

Maneno haya ya Rais Samia yanabeba uzito kwa viongozi wote nchini wenye dhamana ya kuwahudumia wananchi, kuwatumikia na kuwa viongozi na sio watawala.

Tunafahamu kuwa katika moja ya mambo yanayozingatiwa na kusisitizwa na Serikali ya Rais Samia ni ukusanyaji wa mapato ili kupata fedha za kuhudumia wananchi.

Katika siku za karibuni, kumeibuka mzozo kati ya watumiaji wa Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli, Mbezi Luis Dar es Salaam na wasimamizi wa kituo hicho kuhusu ushushaji na upakiaji wa abiria kituoni hapo.

Watumiaji wa usafiri wa mabasi yanayofika Dar es Salaam kutoka mikoani wamelalamika abiria wote kulazimishwa kushuka kituoni hapo na kuzuia mabasi kupakia abiria kwenye ofisi za mabasi husika nje ya kituo.

Jambo hili limeleta usumbufu kwa wasafiri hao wanaotumia mabasi ambayo yana vituo vyao nje ya kituo hicho na hasa pembezoni mwa mji huo wa kibiashara nchini.

Nia ya serikali kujenga kituo hicho ilikuwa nzuri na kwa hakika imeleta unafuu mkubwa kwa wasafiri kwani kituo hicho ni kikubwa na cha kisasa kinachoendana na hadhi ya Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla.

Lakini suala hilo la mabasi kushusha hapo na pia kushusha nje ya vituo vyao linapaswa kutazamwa na kushughulikiwa kwa busara na mamlaka husika, bila kuathiri mapato na bila kuwapa mzigo wananchi.

Tunafahamu wananchi wengi wanafurahia huduma hizo za mabasi hayo kwa kuanzia au kumalizia safari katika vituo ambavyo viko nje ya mji, hivyo kuwaondolea adha ya kushuka au kuanzia Mbezi Luis moja kwa moja.

Tumefarijika na hatua ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla kuingilia kati na kusitisha utaratibu wa kulazimisha mabasi kupakia au kushusha katika vituo vyao, na kuelekeza mamlaka husika kukaa na wamiliki na kuona njia bora ya ukusanyaji mapato.

Kwa kuwa utaratibu wa kuwapo kwa vituo vya nje ya Kituo Kikuu cha Magufuli unakubalika kwa mujibu wa sheria na taratibu, ni vyema kama alivyoeleza mkuu wa mkoa, wahusika kusimamia utekelezaji wake bila kuwa kikwazo au bughudha kwa wasafiri nchini.

Tunaamini waliopewa dhamana hiyo watatumia taratibu na sheria zilizopo kulisimamia hili, huku wakirejea kile alichoeleza Rais Samia kuwahudumia wananchi kwa kuzingatia utawala bora na kurahisisha huduma kwao.

 

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button