Watia nia Iringa Mjini wachuana ridhaa kwa wajumbe

IRINGA: Katika mchakato unaoendelea wa kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wagombea sita wa nafasi ya ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini wameendelea kuwasha moto wa kisiasa kwa kuwasilisha sera na maono yao mbele ya wajumbe wa chama katika kata mbalimbali.

Miongoni mwa wagombea hao ni wabunge wa zamani waliowahi kulitumikia jimbo hilo kwa nyakati tofauti—Mchungaji Peter Msigwa na Jesca Msambatavangu—ambao sasa wanachuana tena kutafuta ridhaa ya kurejea bungeni kupitia tiketi ya CCM.

Msigwa: Nimetoka kwa mama wa kambo, nipo kwa mama mzazi

Mchungaji Peter Msigwa, ambaye alihudumu kama mbunge kupitia CHADEMA kwa zaidi ya muongo mmoja, sasa akiwa kada wa CCM, ameahidi kuwa endapo atapewa nafasi hiyo atafanya kazi kwa karibu na Serikali, tofauti na zamani ambapo alikuwa “upande wa mama wa kambo”.

“Nimewahi kupambana kutatua changamoto zenu nikiwa upinzani. Sasa nikiwa ndani ya chama tawala, nitazitatua kwa wepesi zaidi. Mimi siwezi kuwa mbunge wa ‘kutopokea simu’, nipo kwa ajili yenu na nitahakikisha fedha za asilimia 10, na Mfuko wa Jimbo zinawanufaisha wananchi wa kawaida, siyo wachache tu,” alisema Msigwa mbele ya wajumbe.

Aidha, aliahidi kuwa sehemu ya mapato yake atayarejesha kwa chama kusaidia utendaji katika ngazi ya kata na matawi.

Jesca Msambatavangu: Naomba nimalizie nilipoanzia

Naye Jesca Msambatavangu, aliyemaliza muda wake kama mbunge wa Iringa Mjini kupitia CCM, aliwaomba wajumbe wampe fursa ya kukamilisha miradi aliyoianzisha, huku akiahidi kuibua mingine mipya kwa manufaa ya wakazi wa jimbo hilo.

“Msifanye makosa. Nimekuwa msemaji wa matatizo ya wananchi kwa miaka mingi, na bado nina nguvu ya kuwatumikia. Naomba ridhaa ili tuendelee na yale mazuri tuliyoanza pamoja,” alisema.
Akiwa katika Kata ya Mivinjeni, Jesca alisisitiza kuendelea kuboresha miundombinu ya elimu, kwa lengo la kuhakikisha watoto wanapata elimu bora.

Moses Ambindwile: Mbunge wa msaada wa kisheria na uchumi

Wakili Moses Ambindwile, naye akijinadi mbele ya wajumbe, alisisitiza umuhimu wa elimu ya sheria kwa wananchi.

Aliahidi kufungua dawati maalum la msaada wa kisheria bure katika ofisi ya mbunge, litakalowahudumia wanyonge, wajane, yatima na watu wenye ulemavu.

“Nitajenga SACCOS ya jimbo itakayotoa mikopo rafiki, bila riba au yenye riba nafuu. Vilevile nitaanzisha Trust Fund kwa ajili ya kusaidia wanawake, vijana na makundi maalum,” alisema Ambindwile.

Aliongeza kuwa moja ya vipaumbele vyake ni kuhakikisha mikopo ya halmashauri inawanufaisha walengwa hasa wanawake na vijana wanaojishughulisha na biashara ndogondogo.

Fadhili Ngajilo: Nataka kuwa Mbunge wa kusikiliza

Fadhili Ngajilo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Mkoa wa Iringa, alisema dhamira yake ya kugombea haichochewi na tamaa ya madaraka bali mapenzi aliyonayo kwa wananchi.

“Ninataka kuwa mbunge wa tofauti; ambaye wananchi watanielewa kupitia kazi zangu. Nitazungumza lugha yao, siyo lugha ya kisiasa,” alisema Ngajilo.

Aliahidi kushughulikia changamoto binafsi za wananchi na kuwa mwakilishi wa kweli anayeishi nao, anayeishi maisha yao na anayesikiliza shida zao.

Nguvu Chengula: Nimekuwa karibu na wananchi wakati wote

Nguvu Chengula alieleza kuwa yeye ndiye mgombea anayefaa kwa kuwa amekuwa bega kwa bega na wananchi kwa muda mrefu, akishiriki shughuli mbalimbali za kijamii na kichama.

“Mtu wa kuaminiwa ni yule aliyepo wakati wote, sio anayekuja wakati wa uchaguzi. Mimi nimekuwa nanyi siku zote, najua matatizo yenu, na nipo tayari kuyafanyia kazi,” alisema Chengula.

Islam Huwel awakilishwa

Kwa upande wake, Islam Huwel hakuweza kuhudhuria kuomba kura zake kutokana na kile kilichoelezwa kuwa yuko katika kazi maalum ya kichama, hivyo aliwakilishwa na Katibu wa CCM Wilaya ambaye aliwasilisha dhamira yake ya kugombea.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button