ASKARI wa Sudan wameripotiwa kuwauwa zaidi ya watu 200 wakiwemo wanawake na watoto, katika siku tatu za mashambulizi kwenye vijiji vya kusini mwa nchi hiyo.
Askari wa Sudan wameripotiwa kuwauwa zaidi ya watu 200 wakiwemo wanawake na watoto, katika siku tatu za mashambulizi kwenye vijiji vya kusini mwa nchi hiyo. Hayo ni kwa mujibu wa shirika la wanasheria linalofuatilia vita nchini humo.
Shirika la Emergency Lawyers limesema vikosi vya wanamgambo wa RSF, ambao wamekuwa vitani kwa karibu miaka miwili na jeshi la Sudan, waliwashambulia raia ambao hawakuwa na silaha katika maeneo ambayo hayakuwa na wanajeshi ya vijiji vya Al-Kadaris na Al-Khelwat, jimbo la White Nile.
Limeongeza kuwa RSF ilifanya vitendo vya mauaji, utekaji na uporaji wa mali wakati wa mashambulizi hayo ya tangu Jumamosi, ambayo pia yalisababisha mamia ya watu kujeruhiwa na wengine kutoweka. Shirika la Emergency Lawyers limesema baadhi ya wakazi walipigwa risasi wakati wakijaribu kuvuka Mto Nile.