Watu 250,000 kuhudhuria maziko ya Papa Francis

VATICAN; TaKRIBANI watu 250,000 wanatarajiwa kuhudhuria maziko ya kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis (88) keshokutwa.
Maelfu ya waombolezaji wameshafika jijini Vatican kutoa heshima za mwisho kwa kiongozi huyo aliyeongoza kanisa hilo tangu mwaka 2013.
Takribani wawakilishi 100 kutoka sehemu mbalimbali duniani wanatarajiwa kuhudhuria maziko hayo.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Vatican jana, zaidi ya waombolezaji 20,000 walifika katika viwanja vya Kanisa la Mtakatifu Petro kushuhudia msafara uliobeba mwili wa kiongozi huyo ukipelekwa kwenye eneo hilo.
Wengi wa walioshuhudia tukio hilo wanatarajiwa kujiunga kwenye foleni kuuona mwili wa Papa Francis.
Jeneza lenye mwili wa kiongozi huyo ulianza kupelekwa katika Kanisa la Mtakatifu Petro jana saa 3:00 asubuhi kwa saa za Roma baada ya sala katika Kanisa la Santa Marta alipokuwa akiishi.
Msafara huo uliongozwa na Kardinali Kevin Farrell ambaye anaiongoza Vatican kwa sasa.
Papa aliagiza azikwe katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Maria mjini Roma. Aliaga dunia Jumatatu saa 1:35 asubuhi kwa saa za Roma katika makazi yake Casa Santa Marta kutokana na kiharusi kilichosababisha apoteze fahamu na mfumo wa mzunguko wa damu kushindwa kufanya kazi.
Ripoti za kitabibu zinaonesha alikuwa na tatizo la mfumo wa kupumua na kisukari.
Aliteuliwa kuwa Kardinali Februari 21, 2001 na Machi 13, 2013 alichaguliwa kuwa Baba Mtakatifu na alichagua jina la Papa Francis. Alikuwa Papa wa 266 na wa kwanza kutoka Amerika ya Kusini.