MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ofisi za Mkoa wa Geita imefanikiwa kuandikisha watu 922,000 kwa ajili ya kupatiwa vitambulisho vya taifa kati yao watu 440,000 ni wakazi wa Wilaya ya Geita.
Ofisa Usajili wa NIDA Geita, Emmanuel Ernest amesema hayo katika hafla ya ugawaji wa vitambulisho kwa watendaji wa kata na mitaa za Halmashauri ya Mji wa Geita.
Amesema mpaka kufikia Desemba 2024 zaidi ya vitambulisho 200,000 vimeshatolewa lakini awamu hii ya ugawaji vitambulisho imekusudia kugawa vitambulisho vingine 600,000 mpaka mwezi Machi 2024.
“Kuhusu utaratibu wa kugawa tutashirikiana na ofisi ya mkuu wa wilaya ambapo tumeweka utaratibu mzuri kushirikiana na watendaji kuhakikisha vitambulisho vinawafikia wananchi kwa haraka,”
“Vitambulisho vikishafika kwenye halmashauri husika, vitapelekwa kwenye ngazi ya kata, vikifika ngazi ya kata vitapelekwa ngazi ya kijiji na mtaa ili wananchi wachukue vitambulisho walipojisajili.
“Matarajio yetu ni kwamba baada ya kugawa vitambulisho ambavyo vipo tayari wengine watahamasika kupata na hivo tutaendelea na zoezi la usajili kwani ni endelevu na halina kikomo.” Amesema.
Emmanuel ametoa angalizo kwa wananchi waliojiandikisha tayari tayari wafike kuchukua vitambulisho vyao kwani huduma zilizokuwa zinatolewa kwa kutumia namba ya NIDA pekee haitakubalika.
“Vitambulisho vilichelewa ndio serikali ikasema tuwape namba watumie kupata huduma lakini baada ya vitambulisho kutoka ndani ya siku 90 kama hautachukua itambulisho ile namba itazuiliwa.
“Lengo sasa ni kwamba mwananchi akachukue kitambulisho chake kwa sababu kuna maeneo mengine atatakiwa apeleke nakala ya kitambulisho halisi na siyo namba.” Amesisitiza Emmanuel.
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Cornel Magembe amesema ugawaji wa vitambulisho unatarajiwa kuwa na ufanisi kwani watendaji waliohusika kuandikisha ndiyo hao watahusika moja kwa moja kuvigawa.
Amesema Halmashauri ya Mji wa Geita yenye kata 13 imepatiwa vitambulisho 75,371 ambavyo vitakwenda kupunguza adha ya kukosekana kwa vitambulisho vya taifa miongoni mwa watu.
Magembe ameelekeza watendaji wa halmashauri kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa na kwa kufuata kanuni, taratibu na sheria za utumishi wa umma ili kufikia malengo yaliyowekwa.