Watu milioni moja wanufaika na Watu Simu

DAR ES SALAAM: KAMPUNI ya Watu Simu imesema imefanikiwa kuwafikia zaidi ya Watanzania milioni moja kupitia huduma yake ya upatikanaji wa simu janja kwa mfumo wa mikopo nafuu, hatua inayodai imechangia kukuza biashara na kuongeza ushiriki wa wananchi katika uchumi wa kidijitali.

Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Meneja wa Mauzo wa Watu Simu, Emmanuel Nchinga, alisema kampuni hiyo inaadhimisha miaka mitano tangu kuanzishwa kwa huduma hiyo huku ikiendelea kupanua wigo wa huduma zake nchini.

Alisema katika kipindi hicho, Watu Simu imewawezesha wateja kutoka sekta mbalimbali kumiliki simu janja kwa masharti nafuu, hali iliyowarahisishia kupata taarifa, kutumia huduma za kifedha kidijitali na kuendesha shughuli zao za biashara kwa ufanisi zaidi.

Nchinga alisema mafanikio hayo yamechangiwa na mtandao wa mawakala wapatao 1,993 waliopo katika mikoa yote ya Tanzania, ikiwemo Arusha, Mwanza, Kagera, Songwe na maeneo mengine, ambao wamekuwa wakirahisisha upatikanaji wa huduma kwa wateja na kuchangia kuongeza fursa za ajira.

Aliongeza kuwa kampuni hiyo itaendelea kusogeza huduma zake karibu na wananchi ili kuwawezesha Watanzania wengi zaidi kumiliki simu janja kwa urahisi, hatua inayotarajiwa kuchochea ukuaji wa biashara ndogo na za kati pamoja na kuongeza ushiriki katika uchumi wa kidijitali.

Pia aliwahimiza wananchi kutembelea banda la Watu Simu katika Maonesho ya Sabasaba ili kupata taarifa zaidi kuhusu huduma zinazotolewa na kampuni hiyo na namna ya kunufaika na fursa mbalimbali zinazopatikana.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button