Watu saba wafa ajali ya gari Karagwe

Watu saba wamekufa na wengine tisa kujeruhiwa baada ya lori kugonga magari mawili ya abiria katika eneo la Kihanga Beria Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Kagera, Brasius Chatanda amesema ajali hiyo imetokea majira ya saa 5 asubuhi ambapo dereva wa lori hilo aina ya Scania T621 EJQ lilikuwa kasi, hivyo kupelekea lori hilo na trela lenye namba za usajili T472EAQ kugonga magari ya abiria aina ya Toyota Hiace na Coaster.
Amesema kuwa Coaster yenye namba za usajili 367 ECP na Hiace yenye namba za usajili T 976 DGD yalikuwa yanafanyiwa ukaguzi na idara ya uhamiaji katika beria hiyo ya mazao.

“Dreva alikuwa katika mwendo Kasi inaonekana ni mgeni wa barabara kwa sababu uchunguzi wetu umebaini kuwa alitoka Mbeya akaleta mchele mtukula na baadaye akapata mzigo akapeleka Karagwe na tayari alikuwa na maparachichi katika gari hiyo hivyo alikuwa katika mwendokasi na mashuhuda wanasema aliwasha taa kuonyesha tahadhari,”amesema Chatanda
Amesema kuwa katika vifo saba wanawake ni wanne mwanaume mmoaj na watoto wawili huku kwa majeruhi wanawake ni watano na wanaume ni wanne na wote wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospital ya Rufaaa ya Mkoa wa Kagera na miili imehifadhiwa hospitalini hapo.
Amesema kuwa jeshi la polisi linaendelea kumtafuta dereva wa lori ambaye ametoroka mara baada ya ajali hivyo ni vyema akajisalimisha kujibu mashitaka yanayomkabili.



