WATU wawili wamekufa na wengine sita wamejeruhiwa baada ya watu wanaoaminika ni wafugaji kuvamia kambi ya Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwenye Kijiji cha Mvinza Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Filemon Makungu alisema mjini Kigoma Jumatatu kuwa uvamizi huo ulifanyika kwenye kambi hiyo iliyopo kwenye Hifadhi ya Msitu wa Makere Kusini mwishoni mwa wiki iliyopita.
Kamanda Makungu aliwataja waliokufa kuwa ni mkazi wa Kijiji Mvinza aliyejulikana kwa jina moja la Salvatory ambaye alikuwa kibarua kwenye shamba hilo la miti la TFS ambaye alichomwa na vitu vyenye ncha kali.
Aidha, alisema juzi polisi wakiwa kwenye ukaguzi wa eneo hilo kuangalia athari ya tukio hilo, maiti ya mtu mwingine ilipatikana, Thomas Alfred aliyekuwa akifanya kazi za vibarua kwenye kambi hiyo ya TFS. Mwili wake ukiwa na majeraha makubwa shingoni.
Aliwataja waliojeruhiwa kwenye tukio hilo kuwa ni Dora Nicolaus na David Lazaro ambao ni watumishi wa Suma JKT wakiwa kwenye kazi ya ulinzi ya kambi hiyo, Amon Moshi mtunza bustani, Ndayishimiye Haruna mkulima wa bustani na Elcado Enos pia mkulima.
Mbali ya mauaji na watu hao kujeruhiwa, pia vitu mbalimbali vimeteketezwa kwa moto likiwamo trekta mali ya TFS, nyumba moja ya tofali za kuchoma iliyoezekwa na bati ikitumika kama ofisi, pikipiki sita za watuhumiwa waliokamatwa kwa kuingia kwenye hifadhi ya msitu kinyume cha sheria, gunia 20 za maharage, gunia 70 za mahindi, gunia 30 muhogo na gunia 20 za mtama.
“Taarifa za awali zinaonesha kuwa siku za karibuni kuna ng’ombe ambao idadi bado haijajulikana ya wafugaji jamii ya Wasukuma walikamatwa na kuchukuliwa na maafisa wa TFS kwa tuhuma za ng’ombe hao kuingizwa kwenye hifadhi ya msitu kwa ajili ya malisho.
“Hivyo vurugu hizo zimekuja kama nia ya watu hao kulipiza kisasi kwa mifugo yao kukamatwa na ndiyo maafa hayo yametokea,” alisema Kamanda Makungu.
Watu watatu wanaoaminika ni sehemu ya wafugaji hao, wamekamatwa na wanashikiliwa na Polisi wakituhumiwa kuhusika na tukio hilo na uchunguzi unaendelea.