Watuhumiwa 6 ‘panya road’ wauawa

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limesema wahalifu sita wa unyang’anyi wa kutumia silaha wamefariki dunia baada ya kujeruhiwa  wakijaribu kuwakabili polisi waliotaka kuwakamata.

Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Jumanne Muliro alisema Jumapili watu hao walijeruhiwa juzi saa 4:15  usiku katika eneo la Makongo area 4.

Kamanda Muliro alisema polisi walipata taarifa kutoka kwa wananchi kuwa kulikuwa na kundi la watu tisa waliokuwa katika gari aina ya Toyota Noah lenye namba za usajili T 260 BEP wakitoka Mabibo wakiwa na mapanga na zana nyingine za kuvunjia na kufanyia uhalifu, wakienda Goba Kinzudi, Wilaya ya Ubungo kuvamia nyumba kadhaa na kupora mali usiku huo.

Alisema polisi walipofika Makongo, walikutana na gari hilo na walipolizuia , watuhumiwa hao walishuka na kuanza kuwatishia kwa mapanga askari polisi wakipinga kukamatwa.

“Na katika mazingira hayo, askari walijihami kwa kufyatua risasi kadhaa hewani lakini wahalifu hao waliendelea kukaidi na kutaka kuwajeruhi polisi, ndipo walishambuliwa, kujeruhiwa na baadaye walipelekwa haraka hospitali lakini walipoteza maisha,”alisema Kamanda Muliro.

Alisema watuhumiwa watatu walikimbia na Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam linawasaka.

Kamanda Muliro alisema uchunguzi wa awali ulibaini kuwa watu wawili kati ya hao, ni viongozi wa kundi hilo na wametambuliwa kwa majina ya Salum Juma Mkwama maarufu babu salum anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 27 na 30 ambaye ni mkazi wa Mbagala.

Alimtaja mtuhumiwa mwingine ni Khalifan  Khalifa mkazi wa Buguruni na kwamba waliwahi kushitakiwa kwa kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha (mapanga) mwaka 2021 na baadaye waliachiwa kwa sababu za kisheria.

“Watuhumiwa hao walikutwa wakiwa na mapanga sita, visu viwili na vifaa vingine
vya kuvunjia nyumba,”alisema  Muliro.

Alisema upelelezi wa awali pia ulibaini kuwa watuhumiwa hao waliotambuliwa majina yao, walidaiwa kushiriki katika tukio la mauaji la Septemba 14 mwaka huu usiku Kawe Malingo na matukio mengine ya kuvunja nyumba usiku, kujeruhi kwa mapanga na kupora mali yaliyotokea siku za karibuni.

Kamanda Muliro alisema Jeshi Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam litaendelea kutekeleza maelekezo ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini,  IJP Camilius Wambura ya kuhakikisha mifumo ya usalama na kisheria inazingatiwa usalama uarejeshwe haraka Dar es Salaam.

“Jeshi linatoa tahadhari kwa wahalifu kuacha mara moja, matukio ya kihalifu na watakaokaidi watakamatwa kwa kadri mazingira ya kisheria yatavyoruhusu na kushughulikiwa kwa mujibu wa kisheria,”alisema.

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button