Watumiaji vyombo vya moto waletewa Bima mpya

DSM: BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa kushirikiana na Total Energies na kampuni ya Bima ya Jubilee Allianz wamezindua kampeni ya Bima Mazima kwa watumiaji wa vyombo vya moto.

Mkurugenzi  wa wateja wadogo na binafsi wa benki ya NBC Elibariki Masuke  akizungumza leo Oktoba 11, 2023 jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi huo amesema, makubaliano waliyoingia na Total Energies na Jubilee Allianz ni kuendesha kampeni ya miezi mitatu  ambapo kutakuwa na mawakala wa NBC kwenye vituo vyote vya Total Energies Tanzania nzima ambao watawakatia wateja bima ya Jubilee.

“Si tu kwenye vituo vya mafuta bali hata kwa mawakala wote wa NBC  nchi nzima watakata bima na kutoa mikopo ya ada ya bima, unakopa na kulipa marejesho kidogo kidogo kwa miezi minne mpaka 10, kama gari lina thamani ya Sh milioni 100 kwa bima ya Comprehensive ni Sh milioni 3.5.” Amesema na kuongeza

“Kwa bima ya ‘third part’ gharama yake ni  Sh 108,000 na kwa magari ambayo yamefungwa GPS kuna punguzo la asilimia tano, hivyo watanzania wachangamkie fursa.”Amesema Masuke.

Amesema pia kuna bima ya ajali ambayo ikitokea mtu yupo ndani ya daladala na bahati mbaya ikapata ajali bima ya chini ni Sh 750,000 na kuendelea kulingana na aina ya bima uliyokata.

“Kama muhusika wa bima ikitokea amefariki, familia yake itapata mkono  wa ple wa Sh milioni 3.” Amesema

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Jubilee Insurance, Dipankar Acharya amesema Bima Mazima ni mkombozi kwa watumiaji wa vyombo vya moto yakiwemo magari makubwa na madogo, bajaji na pikipiki.

“Mtu yoyote mwenye kuendesha chombo cha moto  ikijikuta kwenye wakati mgumu sana kibiashara na kiuchumi iwapo hawatakuwa wamejikatia bima ya aina hii,” alieleza.

Amesema, lengo la Jubilee ni kufikia viwango vya juu zaidi na kwamba huu ni mwanzo tu.

Nae, Mkurugenzi wa Sheria na Uhusiano wa kampuni hiyo Getrude Mpangile wa Total Energies amesema  waendesha vyombo vya moto ambao watakata bima ya kuanzia Sh 400,000 na kujaza  mafuta katika vituo vya Total Energies watapata fursa ya kufanyiwa ukaguzi wa magari bure, kupatiwa msaada sehemu yoyote na muda wowote wanapopata changamoto ya kuharibikiwa gari barabarani au tatizo lolote lile.

“Ushirikiano huu ni muendelezo wa kuvifanya vituo vyetu kuwa jumuishi, mteja hataishia kujaza mafuta tu, atapata na huduma nyingine, mafuta yetu yana viambata vya kusafisha injini na pia tuna vilainishi, tuna huduma za kuosha magari, kubadilisha oil na huduma za kifedha.”Amesema Getrude.

 

Habari Zifananazo

Back to top button