Watumishi waagizwa kanuni kuleta tija

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Laban Thomas

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Laban Thomas, amewaagiza watumishi wa umma kuhakikisha wanafanya kazi  kwa kufuata sera, sheria, taratibu na miongozo ya kiutumishi .

Alisema wakifuata taratibu wataweza kuwatumikia wananchi kwa ufanisi na hivyo kuleta tija sehemu za kazi.

Laban ametoa maagizo hayo mwishoni wakati akizungumza na watumishi wa umma  na madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo, katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika mjini Namtumbo.

Advertisement

Aidha amehimiza watumishi hao kufanya kazi kwa ushirikiano, kuacha majungu na kuishi kwa upendo  wakati wote wakiwa kazini na nje ya kazi.

Katika hatua nyingine,Mkuu wa Mkoa amemwagiza Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Chiriku Chilumba kuhakikisha watumishi wanapata haki zao za msingi  za kiutumishi, yakiwemo madai na stahiki  mbalimbali.

“Natoa wiki mbili kwa DED  kuleta taarifa ofisini kwangu ni watumishi wangapi wameshalipwa haki zao na wangapi hawajalipwa kwa nini hawajalipwa,’’alisema.

Aliwataka wananchi na watumishi kulinda miradi ya maendeleo kwani serikali imetoa Sh bilioni 11 ili kutekeleza miradi katika Halmashauri ya Namtumbo.

Aidha amekemea tabia ya udokozi wa mali ya umma kwa baadhi ya watumishina kuwataka wahakikishe wanasimamia ipasavyo miradi yote ya maendeleo iliyopangwa kutekelezwa.

Akizungumzia ukusanyaji wa mapatio, mkuu huyol wa mkoa alisema Wilaya ya Namtumbo ina mazao mengi kama ufuta, mbaazi,soya na mpunga  na kuwataka watendaji wa kata na vijiji wanaokusanya pesa kwa kutumia POS kusimamiwa ili kuhakikisha pesa zote zinaingia serikalini.

Naye Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Chilumba, ameahidi kutekeleza maagizo na kuwasimamia watumishi wa umma  ili watekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria na miongozo ya kiutumishi.