UMOJA wa Wavunaji Misitu katika shamba la miti la serikali la Saohill (UWASA) umemchagua Chesco Ng’umbi maarufu kama CF kuwa mwenyekiti wake mpya na kumtaka ahakikishe mazao ya miti, zikiwemo mbao yanapata bei elekezi.
Ng’umbi ambaye ni mkurugenzi wa makampuni ya CF Ng’umbi Investment amechaguliwa kwa asilimia 99 ya kura 114 zilizopigwa baada ya kukosa mpinzani.
Wengine waliochaguliwa kushirikiana na Mwenyekiti huyo kutekeleza majukumu ya umoja huo ni pamoja na Obadia Kalenga aliyechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti huku Fred Sentam akiteuliwa kuwa katibu.
Akizungumza baada ya kuchaguliwa kushika nafasi hiyo, Ng’umbi amewatoa hofu wavunaji akisema uongozi wake utaendelea kufuatilia changamoto zao na kuwa kiungo kati yao na serikali katika ngazi mbalimbali.
“MIiongoni mwa masuala tutakayoyapa kipaumbele katika uongozi wetu ni kuhakikisha soko la mbao zinazotoka Iringa linakuwa la uhakika ndani na nje ya nchi,” alisema.
Akizungumza umuhimu wa kupata bei elekezi ya mbao hasa katika mikoa ya Iringa na Njombe alisema jambo hilo watalipigania kwa kuwa linalenga kuhakikisha wavunaji wanapata faida inayostahili katika biashara yao.
Kwa kushirikiana na serikali na wadau, Ng’umbi alisema watashauriana pia namna ya kufanya maboresho katika sekta hiyo ya uvunaji ikiwa ni pamoja na kupambana na tishio la kumalizika kwa malighafi za misitu kutokana na uvunaji holela.
“Tutaishauri serikali ichukue hatua ya kuwawezesha wananchi kumiliki ardhi kwa ajili ya kilimo cha miti ili kiwe endelevu na kuondokana na tatizo la kutegemea mashamba ya serikali pekee kupata malighafi hiyo,” alisema.
Kwa upande wake, aliyekuwa katibu wa umoja huo, Dk Basil Tweve, alizungumzia mtikisiko wa soko la mazao ya misitu nchini akiutaka uongozi huo mpya kushughulikia hali hiyo ili kuzuia wadau wengine kuacha biashara hiyo kutokana na hasara wanayopata sokoni.
Naye mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Christian Ahia alisema kwa kushirikiana na serikali na wadau wamefanikiwa kuongeza idadi ya wavunaji ambao sehemu yake wanapata vibali vya kuvuna katika mashamba ya serikali.
Lakini pia amesisitiza umuhimu wa kuangazia pia wavunaji wadogo na suala la mikataba yao ili kuhakikisha wanakuwa na uhakika wa biashara yao na sio kuondolewa kwenye shughuli hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya serikali katika uchaguzi huo Katibu Tawala wa Wilaya ya Mufindi, Frank Sichawe ametaka chama hicho kuimarisha utulivu na kuheshimu katiba ili kutoyumbisha sekta ya misitu na kuhakikisha serikali inakusanya kodi yake kwa uhakika.