Wawekezaji mawasiliano kuendelea kuungwa mkono

Wawekezaji mawasiliano kuendelea kuungwa mkono

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, amesema Serikali itaendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na wawekezaji katika sekta ya mawasiliano ambao wanaleta mageuzi.

Waziri Nape amesema hayo jijini Dar es Salaam alipotembelea kituo cha mkongo wa mawasiliano cha 2 Afrika kinachosimamiwa na Kampuni ya Airtel, ambapo kukamilika kwake kutawezesha kuunganisha nchi zaidi ya 30 Afrika.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, akizungumza wakati wa hafla yake fupi ya kutembelea kituo cha Uendeshaji Mkongo wa Mawasiliano cha 2 Afrika kinachomilikiwa na Kampuni ya Airtel Tanzania kilichopo Mbezi jijini Dar es Salaam leo 24 Machi, 2023.

“Kwanza niwapongeze Airtel kwa kuliona hili ambalo litaleta mageuzi makubwa kwenye sekta ya mawasiliano, mkongo huu utakuwa wenye kasi zaidi na utasaidia kuunganisha watu kwa mataifa tofauti, hivyo naamini utatatua kwa kiwango kikubwa changamoto za kimawasiliano,” amesema Waziri Nape.

Advertisement

Waziri Nape ameongeza kuwa kuongezeka kwa mkongo uliopita chini ya bahari ni dalili nzuri, kwani watoa huduma kama vile mitandao ya simu watakuwa na nafasi ya kufanya machaguo juu ya mkongo upi utumike kitu ambacho kinaweza kuchangia kushuka kwa gharama na kuongezeka kwa ubora wa huduma za Intaneti.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Airtel, Dinesh Balsingh amesema mkongo huo utakuwa mkombozi na utaleta mageuzi makubwa katika sekta ya mawasiliano.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Selestine Gervas Kakele akipata maelezo juu ya ufanyaji kazi wa kituo cha Uendeshaji Mkongo wa Mawasiliano cha 2 Afrika kinachomilikiwa na Kampuni ya Airtel Tanzania kilichopo Mbezi jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya Waziri wa Wizara hiyo. Nape Nnauye kituoni hapo leo 24 Machi, 2023.

 “Tunaendelea kushirikiana na serikali katika kuhakikisha mwananchi anapata unafuu katika mawasiliano, hivyo kampuni zote za mawasiliano zinaweza kutumia mkongo huu ili tuzidi kumpunguzia gharama mwananchi”-amesema Dinesh

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *