Wawili kufanyiwa upasuaji wa marudio nyonga, magoti

DAR ES SALAAM: TAKRIBANI wataalamu wa mifupa 80 kutoka China na Tanzania wamekutana jijini Dar es Salaam katika kongamano la Kisayansi kati ya nchi hizo mbili yenye lengo la kubadilishana uzoefu, maarifa, ubunifu na matumizi ya teknolojia .
Aidha katika Kongamano hili wagonjwa wawili wanatarajiwa kupandikizwa nyonga na magoti kwa marudio katika Hospitali ya Muhimbili – Mloganzila.
Akizungumza katika kongamano kwa niaba ya Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili –Mloganzila Profesa Mohammed Janabi, Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji, Dk Godlove Mfuko amesema kongamano hilo limejikita katika ubunifu mpya katika vifaa vya kubadilisha nyonga, magoti na upasuaji.
SOMA ZAIDI: Saba wapandikizwa nyonga, magoti Mloganzila
“Kuna wataalamu kutoka hospitali kubwa za huko wamekuja kubadilishana uzoefu na wataalamu wa ndani lakini pia kuangalia fursa kwamba wataalamu wetu wanaweza kwenda China kujifunza zaidi.
Ameongeza kuwa: “Hapa leo tunajadili kwa kuangalia tafiti, teknolojia na upasuaji mbalimbali, lakini kesho Mei 18,2025 kutakuwa na upasuaji wa kubadilisha nyonga na magoti kwa wagonjwa wawili ambapo wataalamu wa China na wa kwetu watapata nafasi ya kufanya upasuaji huo kwa watanzania na itakuwa fursa kwa madaktari wa ndani.
Amesema upasuaji unachukua saa tatu endapo vifaa vikiwepo na kwamba wameshafanya upasuaji wa marudio kwa wagonjwa saba na vifaa vikipatikana inafanyika kwa urahisi.
SOMA ZAIDI: Mloganzila yaandaa kambi kupandikiza nyonga, magoti
Mkurugenzi wa Tiba Wizara ya Afya, Dk Hamad Nyembea amesema Tanzania ni eneo la tiba za kibingwa ambapo inajitahidi sana kupata mabingwa ambapo hapo wamekutana kujadiliana namna ya kuboresha huduma za kibobezi na wamejikita hapa katika huduma za mifupa hasa upasuaji wa nyonga.
“Kwa upande wa uwekezaji madaktari bingwa wa mifupa sasa wanapatikana nchi nzima na kuna huduma nyingi za kibingwa mfano hii ya kubadisha nyonga na magoti inafanyika sasa hapa kwetu japo bado ni changamoto.
Dk Nyembea amesema kutokana na changamoto kadhaa zilizopo wameamua kushirikiana na wataalamu wa China ili kupata utaalamu zaidi na teknolojia zilizopo katika nchi zilizoendelea .
“Na baada ya kujifunza wataalamu wetu wataanza kufanya wenyewe.
Professa Cao Li kutoka China amebainisha kuwa Tanzania na China wana historia ya muda mrefu kwahivyo wanataka uhusiano mzuri zaidi kuendelezwa.
“Mimi ni daktari wa upasuaji ninamaarifa na uzoefu hasa Tanzania inahitaji hii ,tumekuja hapa kubadilishana uzoefu na kubadilishana maarifa na wataalamu wa Tanzania naamini wagonjwa wa hapa nyumbani watapata faida kutoka katika haya mabadilishao ,”amesisitiza prof Li