WATU wawili wamekufa kufuatia ajali ya ndege mbili zilizogongana angani na kuamgukia katika Mbuga ya Kitaifa Nairobi nchini Kenya.
Waliofariki wanaripotiwa kuwa rubani mwanafunzi na mkufunzi waliokuwa ndani ya ndege aina ya Cessna mali ya Ninety-Nines Flying School.
Ndege ya pili, Dash 8, ni ya Safarilink Aviation Limited ambayo imethibitisha kuwa ilikuwa ikielekea Diani ikiwa na abiria 39 na wafanyakazi watano ilipata kishindo mara baada ya kupaa.
Hakuna vifo vilivyoripotiwa kutoka katika ndege ya shirika la Safarilink.
“Safarilink Aviation inapenda kutoa taarifa kwamba asubuhi ya leo saa 9:45 kwa saa za ndani, ndege yetu nambari 053 ikiwa na abiria 39 na wafanyakazi 5 waliokuwa wakielekea Diani ilipata kishindo kikubwa mara baada ya kupaa. Wafanyakazi waliamua kurejea Nairobi mara moja uwanja wa ndege wa Wilson kwa ukaguzi na tathmini zaidi,” ilisema taarifa ya Safarilink.