Watakiwa kushiriki kampeni chanjo dhidi ya surua

DAR ES SALAAM, Serikali kupitia Wizara ya Afya, imetoa wito kwa wazazi, walezi, na walimu kushiriki kikamilifu katika kampeni ya chanjo dhidi ya magonjwa ya surua na rubela, kuanzia mwezi wa pili, jitihada hii inalenga kuimarisha kinga ya watoto na kuzuia kuenea kwa magonjwa ya milipuko. Jitokezeni kwa wingi kwa ajili ya afya bora ya jamii yetu!

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa mwaka wa kutathimini huduma za chanjo nchini kwa mwaka 2023, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Grace Magembe, amewahimiza wananchi kufanya usafi wa mazingira ili kuepukana na magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu.

“Ni jukumu la wananchi kujikinga na maradhi ya milipuko kwa kufanya usafi wa mazingira, kunawa mikono, na kuzingatia kanuni za afya, hasa wakati wa kuwapatia watoto chakula,” amesisitiza Dk Magembe.

Aidha, amepongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ya kununua vifaa vya afya, huku akisisitiza umuhimu wa watumishi kutoa taarifa sahihi na kuzingatia maadili katika kutoa huduma kwa wananchi.

Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Tumaini Nagu, ameonya kuwa mikoa takribani nane tayari ina maambukizi ya kipindupindu na amewataka waganga wakuu wa mikoa kusimamia afua za usafi kuhakikisha miundombinu ya kunawia mikono inakidhi viwango vya kukabiliana na magonjwa.

Serikali inaendelea kutoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika kampeni hii muhimu ya chanjo ili kujenga kinga imara na kuepukana na athari za magonjwa ya milipuko.

Habari Zifananazo

Back to top button