MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Arusha, Willfred Ole Soileli amewaomba wazee wa kata ya Moshono ndani ya Jiji la Arusha kuitumia vema mashine ya kusaga na kukoboa yenye thamani ya Sh milioni 11 kujikomboa kiuchumi.
Soileli alisema hayo wakati akiwakabidhi wazee hao mashine hiyo iliyotolewa kwa msaada na Kiongozi Mkuu Tanzania wa Kanisa la Kilokole linajulikana kwa jina la Kanisa Halisi, Baba Halisi sherehe ya makabidhiano ilifanyika katika uwanja wa shule ya msingi Moshono jana.
Alisema kiongozi wa Kanisa hilo Tanzania amewiwa na kuamua Kuwasaidia wazee wa kata ya Moshono mradi huo wa mashine hivyo wazee nao wanapaswa kujipanga kuhakikisha mashine hiyo inawakwamua kiuchumi.
Mwenyekiti alimwomba kiongozi wa kanisa hilo kuangalia namna ya kuwasaidia wazee wengine wa kata nyingine ndani ya Jiji la Arusha ili nao waweze kujikwamua kiuchumi.
Baba Halisi alisema kuwa dhahebu lake liliamua kutoa msaada huo kwa wazee wa kata ya Moshono bila kuombwa na mtu wala kiongozi yoyote Ila kanisa lake liliamua kufanya hivyo kama Mwenyezi Mungu alivyomwongoza.
Alisema kuwa Moshono ni sehemu ya Tawi lake la Kanisa na wazee wa Moshono walimpa ushirikiano sana katika shughuli za maombi hivyo naye ameamua kuwakumbuka Kwa kuwapa mashine hiyo ili iweze Kuwasaidia katika kujikimu katika Maisha yao.
Naye Diwani wa Kata ya Moshono ,Miryamu Kissawike alimshukuru sana Kiongozi Mkuu Tanzania wa Kanisa hilo,Baba Halisi na kusema kuwa msaada huo kwa wazee wa Moshono ni msaada mkubwa sana kwani Wazee wa Kata hiyo sasa watajikomboa kiuchumi.
Alisema yeye binafsi ameshawatafutia sehemu ya kujenga na kuweka mradi huo na pia atawatafutia Meneja mradi Na mhasibu Kwa ajili ya utunzaji wa fedha za mradi na kamwe hatakuhali kuona mradi huo unakufa kwani atakuwa mstari wa mbele kuhakikisha mradi huo unaendelezwa Kwa maslahi ya wazee wa kata ya Moshono na sio vinginevyo.
Diwani aliwataka wazee wa Moshono kuulinda mradi Kwa maslahi yao na kuacha mara moja kuingiza mradi huo katika masuala ya kisiasa kwani sio sehemu yake na hilo atalisimamia Kwa nguvu zote.
Naye Mzee Pascal Laizer amemshukuru Diwani wa Kata ya Moshono na kiongozi wa kanisa kwa kufanikisha mradi huo kwa kuwakumbuka wazee na kusema kuwa Mwenyezi Mungu atawalipa na wao wataulinda mradi huo ili iweze Kuwasaidia katika Maisha yao ya kila siku tofauti na awali.