Wazee Missenyi wavutiwa msaada wa kisheria Mama Samia

KAGERA: BAADHI ya wazee wilayani Missenyi wamepoingeza Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia na kudai kuwa imeleta mwanga mkubwa juu ya changamoto za ufahamamu kuhusu maswala ya umiliki wa ardhi, kuandika wosia pamoja kuandaa wasimamizi wa mirathi.
Kampeini ya Msaada wa Kisheria wilayani Missenyi imeingia siku ya tatu ikiwa inaangazia utatuzi wa migogoro ya kisheria, usaidizi wa kisheria pamoja na utoaji wa elimu ya kisheria upande wa mirathi, wosia, ukatili, ardhi, malezi, ajira na madai.
Alexander Kayombo mkazi wa kijiji cha Bubale kata Kakunyu wilayani Missenyi amesema moja ya changamoto kubwa kwa sasa kwa wazee ni ukatili na unyanganyi juu ya maswala ya ardhi pamoja na ukosefu wa elimu kwa vijana wadogo ambao wanaongoza kwa kuvunja sheria.
“Nina miaka 78 ,sijawai kufuatwa wa wakili au mwanasheria kuja kijijini kutsikiliza kwa mara ya kwanza nimeona serikali imetuma mawakili kwa kijiji cha mpakani kuja kutoa elimu na kupokea changamoto za kisheria bila kwenda kusimama kizimbani hii ni hatua kubwa sana kwetu ,pamoja na miradi mikubwa tunayoona lakini hili ni swala la kugusa hisia za mtu moja kwa moja na ni faraja,” amesema.

Leonia Aloyce ,90, mkazi wa Missenyi ameguswa na elimu ya usimamizi wa mirathi kisheria na kudai kuwa haijawai kutokea wananchi kupata elimu usimamizi wa mirathi na wengi wanadhani kuwa familia zenye wasimamizi wa mirathi ni familia zenye uwezo.
Aidha wananchi wa Bubare wamepongeza hatua za Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi kuangazia kijiji chao na kuwahaidi wananchi kuwa kijiji hicho kiko kwenye mipango ya kuwapatia hati wananchi wake kwa sababu ni moja ya Kijiji kinachokua.
Akitoa elimu ya kisheria juu ya maswala ya ardhi Ofisa Mipango Miji na Vijiji wilayani Missenyi Deliqueen Lyimo amesema kuwa kijiji hicho kimeonekana kuwa kinakua kwa Kasi hivyo halmashauri Iko tayari kuanza kutoa hati miliki za viwanja kwa mujibu Sheria No 4 ya Ardhi ya Mwaka 1994 na wengine ambao maeneo yao hayajakua watapata hati za kimila kwa mujibu wa Sheria No 5 ya Ardhi ya Mwaka 1999.

“Tayari tumepima kijiji chenu na tumeona kinakua kwa kasi ndio maana leo kupitia kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia tunatoa elimu za umiliki wa ardhi na maswala ya hati ili muelewe kuwa mama amedhamilia kuwaokoa wananchi wenu na watoto wenu kwa sababu ardhi ikishamilikiwa haifutwi na mtu unaweza kutumia ardhi yako kufanya biashara,kukopa ,na kufanya uwekezaji,”amesema Lyimo.

Hatua hiyo na elimu juu ya maswala ya hati imefurahisha vijana wazee na wananchi wa Bubale kwa ujumla na kudai kuwa hiyo ni habari njema na hawatachezea fursa juu ya kumiliki maeneo yao kihalali.
Mratibu wa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia Missenyi, Maxmillan Fransis amesema kuwa ndani ya siku 3 mfululizo maswala yaliyojitokeza katika wilaya hiyo yanayohitaji utatuzi wa haraka ni mirathi pamoja na changamoto za ardh.



