DAR ES SALAAM: BARAZA la Ushauri la Wazee Taifa wametaka dira iweke suala la kutungwa na kuanzishwa kwa sheria ya wazee nchini ili kuenzi na kuratibu masuala mbalimbali yatakayoinua ustawi wao.
Hayo yamesemwa Dar es salaam leo Desemba 22, 2024 wakati wakitoa maoni yao katika Mkutano wa Kuhakiki Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 wa Baraza la Ushauri la Wazee Taifa.
Aidha, Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Wazee Taifa, David Lameck Sendo amesema ili kukamilisha kuandikwa kwa Dira hiyo, wazee wametaka kuimarishwa kwa mifumo na taasisi za ustawi wa jamii nchini ikiwamo kuanzishwa kwa sheria ya huduma za ustawi wa jamii ili kuimarisha uratibu na usimamizi wa huduma ikiwamo za wazee.
Pia amesema wamependekeza kukamilishwa kwa Sera ya Wazee nchini, kutoa kipaumbele cha bajeti za huduma ya wastawi wa jamii, kuanzishwa kwa idara ya ustawi wa jamii inayojitegemea kuanzia ngazi ya wizara, mikoa na Halmashauri ili kuimarisha huduma za ustawi wa jamii kwa wazee na makundi mengine.
Sendo amesema dira ioneshe kuimarishwa kwa mifumo kwa familia, malezi na makuzi bora ya watoto yenye kuzingatia maadili na miiko ya taifa la Tanzania, na kuimarishwa kwa mifumo ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya wazee, watoto na kuwa na Mpango wa Taifa wa Kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake.
Pia Sendo amesema kwenye shabaha ya jumla ya dira waweke kuboresha ustawi wa wazee kwani hawajapewa kipaumbele katika dira ni sawa na kuonekana kuwa wazee hawana uhai katika dira hiyo.
Aidha Sendo amesema kuwa wazee wanahitaji Mabaraza ya Wazee kujengewa uwezo ili kutekeleza majukumu kikamilifu ikiwamo kutoa ushauri kwa jamii, kulinda mila na desturi. Halikadhalika wametaka kuwepo kwa sheria ya wazee itakayowawezesha upatikanaji na utekelezaji wa huduma kwa wazee kama stahiki ya leo kwa mujibu wa Sera ya Wazee na Sera nyingine.
Pia wamependekeza kuelekea mwaka 2050, wazee nchini wameomba kuwa katika Bima ya Afya kwa Wote, kundi la wazee litambuliwe kwa kupatiwa bima maalumu ili kuthamini mchango wao katika maendeleo ya taifa.
Katibu wa Baraza la Ushauri la Wazee Taifa, Anderson Lyimo ameshauri serikali iangalie umuhimu wa kuthamini kundi la wazee, pia aliomba wazee watajwe kwenye wizara husika na sio kwenye kundi maalumu.
Lyimo amesema wazee wengi wanaishi vijijini lakini wanaishi katika mazingira magumu hivyo waliomba ili kutendewa haki wafanye sensa kuangalia ni wazee wangapi wanaoishi katika mazingira magumu ili waweze kuwapa msaada wa kiuchumi.
Pia kwa upande wake amesema wazee wanaathirika kwa magonjwa sana, hivyo walishauri kuwa wazee ambao haaana bima wapate bima ya afya maalumu kwa ajili ya kupatiwa matibabu bure na kanuni ziwekwe wazi kuwa mzee atapataje matibabu bure kupitia bima hiyo.
Wamesisitiza dira iweke mikakati ya kuimarisha ulinzi na usalama na kupinga ukatili dhidi ya wazee, na adhabu kali zichukuliwe dhidi ya watakaobainika kufanya ukatili dhidi ya wazee.