Waziri ashusha kibano TRC
KIGOMA; Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amelitaka Shirika la Reli nchini (TRC), kubadilisha mtazamo wa utendaji kazi wake, ili kuleta ufanisi na kuondoa changamoto nyingi zinazojitokeza katika kuwahudumia wateja.
Waziri Mbarawa amesema hayo mjini Kigoma akizungumza na wafanyakazi wa TRC katika kituo cha reli cha Kigoma na kusema kuwa utendaji wa sasa wa shirika hilo umelifanya kuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wateja sambamba na malalamiko ya kucheleweshwa malipo ya watumishi.
Alisema kuwa kuanzia sasa viongozi na watumishi wa TRC ni lazima wabadilike na kujituma zaidi sambamba na uongozi kubuni na kuweka mikakati ambayo itaongeza ufanisi na faida kwa shirika na badala yake kama mtu hawezi kwenda na kasi hiyo ajiondoe au serikali itamuondoa na kuleta watumishi wengine.
Waziri huyo wa uchukuzi ameeleza kushangazwa na hali hiyo ya utendaji katika kusafirisha mizigo ya abiria, ambapo treni ya mizigo inaweza kuchukua mwezi mmoja kutoka Tanga hadi Kigoma jambo ambalo kwa namna yeytoe haliwezi kuliingizia faida shirika.
Akizungumza kuhusu kauli hiyo ya Waziri Mbarawa, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Senzige Kisenge amesema kuwa wamepokea maelekezo ya Waziri na watayafanyia kazi kuleta ufanisi wa shirika.
Kisenge alisema kuwa wakati huu ambapo shirika limekuwa na miradi mikubwa ya ujenzi wa njia za reli na kuleta treni za mwendo kasi, ni wazi mabadiliko makubwa ya usimamizi na kiutendaji yanahitajika hivyo wanapokea maelekezo hayo na kuyafanyia kazi kikamilifu ili kulifanya shirika kuwa na ufanisi mkubwa.



