Waziri Kabudi aagiza mageuzi TSN

DAR ES SALAAM –– Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi, amezindua bodi mpya ya Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) na kuielekeza kuharakisha maandalizi ya sheria yatakayowezesha kuanzishwa kwa Shirika la Magazeti la Serikali.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa bodi hiyo, iliyofanyika Ijumaa, Agosti 8, Prof. Kabudi aliitaka bodi hiyo, inayoongozwa na Inspekta Jenerali wa Polisi mstaafu Said Mwema, kufanya mapitio ya muonekano wa magazeti ya Daily News na HabariLEO, ambayo yamekuwa yakichapishwa tangu Januari 1972 na Desemba 2006 mtawalia.
Amesema bodi hiyo pia inapaswa kuendelea kusimamia menejimenti ya kampuni ili kutimiza mpango wa upanuzi wa mradi wa kiwanda cha uchapishaji kibiashara, hatua itakayoiwezesha TSN kuchapisha magazeti na machapisho mengine kwa ufanisi na ushindani.
Prof. Kabudi ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuimarisha uhuru wa habari nchini, hatua iliyoiwezesha Tanzania kupanda nafasi katika viwango vya kimataifa vya uhuru wa habari. “Uhuru wa habari ni pamoja na vyombo vya habari vya umma kama TSN na TBC. Navyo vinahitaji uhuru wa uhariri unaowajibika,” amesisitiza Waziri Kabudi.
Aidha, amemshukuru Rais Samia kwa kuwekeza kwenye TSN kwa kutoa fedha na ajira mpya, sambamba na uteuzi wa IGP mstaafu Mwema, ambaye amemwelezea kama kiongozi mabadiliko. “Amefanya mageuzi makubwa akiwa Kiongozi wa Jeshi la Polisi. Tuna imani kuwa ataiongoza TSN kwa weledi na kuwa kiongozi wa timu yenye matokeo,” amesema Prof. Kabudi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti mpya wa Bodi ya TSN, Said Mwema, ameahidi kushirikiana na wajumbe wa bodi kubadili changamoto zinazokikabili chombo hicho cha habari kuwa fursa. “Muhimu ni kuiwezesha TSN kuwa daraja na si ukuta,” amesema IGP mstaafu Mwema.

Mwenyekiti wa zamani wa TSN, Hab Mkwizu, amepongeza jitihada za Serikali kuendeleza chombo hicho, akibainisha kuwa bodi iliyomaliza muda wake imefanya juhudi kubwa zilizosaidia kuboresha hali ya TSN. “Tuliikuta TSN katika hali mbaya, leo tunaondoka tukiiacha ikiwa na hesabu safi na mwelekeo mzuri,” amesema Mkwizu, ambaye pia ni Katibu Mkuu mstaafu wa Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma.
Awali Kabudi, amezindua Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) yenye wajumbe saba akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni, Bi Asha Dachi.
Bodi hiyo itakayoongozwa na Mwenyekiti, Inspekta Jenerali wa Polisi mstaafu, Said Mwema, imeanza kazi rasmi baada ya kuzinduliwa leo Agosti 8, katika ofisi za Kampuni ya Magazeti TSN zilizopo Tazara, Temeke mkoani Dar es Salaam. Hafla hiyo pia imehudhuliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa.
Wajumbe wa bodi hiyo ni pamoja na Dk. Chisugilie Salum Khadudu, Mkufunzi katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT); Bi. Joseline Jonathan Kamuhanda, Mkuu wa Kitengo cha Masoko, Benki ya CRDB; Dk. Ayub Rioba Chacha, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC); na Bi. Elimbora Abia Muro, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Ndani katika Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA).
Wengine ni Bw. Deogratius Charles Kwiyukwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo Tanzania (TIB); na Bi. Zamaradi Rashid Kawawa, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari Maelezo, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.