Waziri Kapinga: DSE kukuza mitaji wafanyabiashara

DODOMA; USHIRIKIANO wa Wizara ya Viwanda na Biashara na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) utaziwezesha biashara nyingi nchini kufikia masoko ya mitaji na kukua, jambo ambalo litaimarisha sekta ya viwanda na kuongeza tija katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, alipokutana na kuzungumza na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Peter Nalitolela, ofisini kwake jijini Dodoma kwa lengo la kukuza ushirikiano kati ya wizara na DSE.

Waziri Kapinga amebainisha kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara ndiyo mhimili wa viwanda na biashara zote, hivyo DSE ina fursa kubwa ya kuwezesha biashara nyingi kupata mitaji na kufikia masoko mapana.
Aidha amewaelekeza viongozi wa Wizara kuweka mipango madhubuti itakayonufaisha sekta ya viwanda kwa maendeleo ya nchi.
Kwa upande wake, Nalitolela, amesema kuwa DSE imejipanga vizuri kujitambulisha kama mdau muhimu wa maendeleo na kuahidi kuwa soko liko tayari kutumika kama daraja la kuimarisha mitaji kwa kampuni za ndani ili kukuza uchumi wa Taifa.

Katika mkakati wa kuelekea uchumi wa dola trilioni moja na Dira ya Taifa ya Mendeleo ya mwaka 2050, amesema DSE imepanga kuongeza idadi ya wawekezaji kufikia milioni moja ifikapo mwisho wa mwaka huu, na kufikia milioni 10 ifikapo mwaka 2032.
Amesema mkakati huo unahusisha kuwashawishi wafanyabiashara wakubwa nchini kujiunga na soko hilo, pamoja na kutoa elimu ya uwekezaji kwa wananchi wengi zaidi.

Amebainisha kuwa Soko la Hisa la Dar es Salaam limepiga hatua kubwa kwa kusajili mashirika ya ndani na nje yenye thamani ya takriban shilingi trilioni 29.



