Waziri Mkuu azindua mpango mkakati wa amref

Asisitiza mashirika yasiyo ya kiserikali kuzingatia maadili

DAR ES SALAAM: Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amezindua Mpango Mkakati wa miaka nane wa AMREF Tanzania na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kufanya ufuatiliaji ili kuhakikisha afua zilizopo katika mpango huo zinatekelezwa kwa ufanisi na kuboresha huduma za afya kwa Watanzania.

Majaliwa amesema kuwa mpango mkakati huo ambao unatarajia kugharimu dola za kimarekani milioni 458 kwa miaka yote nane utajikita katika kuboresha Afya ya msingi ikiwemo, kutekeleza afua za afya ya uzazi pamoja na afya ya mama na mtoto, afua za magonjwa yasiyoambukiza utasaidia katika kuimarisha afya na ustawi wa Watanzania

Ameyasema hayo, Septemba 15, 2023 wakati akizindua mpango huo katika Hoteli ya Serena, Dar Es Salaam. Mpango mkakati huo kuanzia mwaka 2023 hadi 2030 ili kuelekea katika malengo ya maendeleo endelevu ya dunia 2030.

“Niwahakikishie kuwa, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Afya Tanzania Bara, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Wizara ya Afya Zanzibar, na wizara nyingine zote ambazo shughuli zenu zinahusiana nazo itaendelea kushirikiana na Amref Tanzania katika utekelezaji wa mpango mkakati huu”

Katika Hatua nyingine Majaliwa ametoa wito kwa Mashirika yasiyo ya Kiserikali, kuzingatia maadili ya nchi wakati wa utekelezaji wa afua mbalimbali.

“Msikubali kutumika kuwa chombo cha kuhamasisha mmomonyoko wa maadili ya Taifa letu. Kila shirika litekeleze majukumu yake kwa kuzingatia mkataba uliopo kati yake na Serikali. ”

Aidha, amezitaka Mamlaka zote za Serikali zinazohusika na usajili wa mashirika yasiyo ya Kiserikali kufuatilia kwa karibu utendaji wa mashirika hayo ili kuzuia mianya ya kuhamasisha vitendo vya mmonyoko wa maadili.

Naye Mkurugenzi Mkazi wa AMREF Tanzania Dkt. Florence Temu amesema gharama za kutekeleza mpango mkakati huo itakuwa inaongezeka mwaka hadi mwaka ambapo kwa mwaka 2023 itakuwa ni Dola za marekani milioni 40 ambayo itakuwa ikikua kwa asilimia 30.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button