WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax amezindua na kuweka Jiwe la Msingi miradi ya miwili ya maendeleo katika Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara mapema hii leo.
Miradi hiyo ni zahanati ya Magomeni na shule ya sekondari ya Tandika ambayo imegharimu Sh milioni 600.
Akizungumza mara baada ya uzinduzi huo, waziri huyo amesema zahanati hiyo ni moja kati ya 270 zinazojengwa mkoani humo.
Waziri Stergomeana amesema: “Zahanati hii ina maana kubwa sana kama hauna afya huwezi kuwa na nguvu na huwezi kufanya shughuli zako za maendeleo.”
Amesema hiyo ni dhamira ya wazi ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwaletea wananchi maendeleo, kudumidha ustawi wa wananchi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanakuwa na afya bora inayohitajika ili waweze kujitegemea wao wenyewe, kujimudu kisha waweze kuchangia shughuli za maendeleo za taifa lao.
SOMA: Waziri Stergomena aanza ziara Mtwara
Amesema serikali ya awamu ya sita imefanya mambo mengi makubwa nchini ikiwa ni pamoja na Mkoa wa mtwara ambao unakwenda kwa kasi kubwa hivyo.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala ameishukuru serikali kwa kuleta miradi mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya Sh bilioni 740.6 kwenye Mkoa huo ambapo kati ya fedha hizo, zaidi ya Sh bilioni 200 imetekeleza miradi ya maendeleo katika Manispaa ya Mtwara mikindani kwa ujumla.
Mkazi wa manispaa hiyo, Zaibanu Mohamed “Tunaishukuru sana serikali yetu kwa kutujengea na kutufungulia miradi ya maendeleo kwenye manispaa yetu na tunajionea sasa mkoa wetu unavyopiga hatua kimaendeleo”
Waziri huyo yuko kwenye ziara ya kikazi ya siku tano mkoani humo kwa ajili ya kutembelea, kuzindua na kuweka jiwe la msingi miradi mbalimbali ya maendeleo katika mkoa huo.